Sudan Yachangiwa Zaidi ya Euro Bilioni Mbili

Zaidi ya euro bilioni mbili za msaada kwa ajili ya Sudan zimechangishwa katika kongamano la wafadhili lililoandaliwa mjini Paris, Ufaransa,hii ni baada ya Ujerumani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya kuiomba jumuiya ya kimataifa kutoa msaada wa dharura kushughulikia hali ya kutisha ya kibinadamu katika nchi hiyo inayokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

 Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema kuwa hawajasahau kinachoendelea Sudan na kueleza kuwa kiwango cha dhamira yao kitawawezesha kuyatimiza mahitaji ya dharura ya chakula, afya, maji, usafi, elimu na ulinzi wa watu walioko hatarini zaidi.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Stéphane Séjourné, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Joseph Borell na Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na Migogoro Janez Lenarcic walihudhuria mkutano huo, pamoja na wawakilishi kutoka asasi za kiraia nchini Sudan.

Akizungumza mjini New York, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huenda umefanywa nchini Sudan. Alitaja mashambulizi ya kiholela yanayouwauwa, kuwajeruhi na kuwahangaisha raia wakati wa mgogoro kati ta jeshi na wanamgambo wa RSF.

Ameongeza kwamba ulimwengu unawasahau watu wa Sudan na kutoa wito wa juhudi za pamoja za kufikiwa mpango wa kusitisha mapigano na kumaliza umwagaji damu. “Tatizo kuu liko wazi: kuna majenerali wawili ambao wameamua kuhusu suluhisho la kijeshi na hadi sasa, wanazuia juhudi zote kuu za upatanishi,” alisisitiza Guterres.

Amebainisha kwamba njia pekee ya kumaliza mzozo huo ni suluhisho la kisiasa katika nchi hiyo ambayo Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini vimeingia mwaka mmoja tangu vilipoanza Arili 15 mwaka wa 2023.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *