STAND UNITED YAWAOMBA WANASHINYANGA KUIPA HAMASA ZAIDI TIMU….

NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA 

WANANCHI wa Shinyanga, wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono Timu ya Stendi United Chama la Wana kwenda nayo mkoani Geita siku ya Jumapili tarehe 12 january 2025 katika mchezo wao dhidi ya Geita Gold, ili kuwapatia hamasa wachezaji na kuibuka na ushindi kwa kuondoka na pointi 3.

Wito huo umetolewa leo Januari 10, 2025 na Mratibu wa Safari hiyo Jackline Isaro wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusiana na mechi hiyo.

Amesema Timu ya Stendi United siku ya Jumapili Januari 12,2025 itakuwa na mchezo wa muhimu dhidi ya Geita Gold katika Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita, na kwamba mdau wa michezo mkoani Shinyanga Mhandisi James Jumbe, ametoa ufadhili wa mabasi ambayo yatabeba mashabiki bure kwenda Geita kwa ajili ya kuiunga mkono timu yao na ili kurudi na ushindi wa point 3.

“Nawaomba Wananchi wa Shinyanga wajitokeze kwa wingi Siku ya Jumapili Alfajiri ili kuondoka kwenda Geita kuiunga mkono Timu yetu ya Stendi United, ilirudi na ushindi wa point 3, ambapo mdau wa Mchezo Mhandisi James Jumbe ametoa Mabasi ya kuwabeba kwenda na kurudi bure,” amesema Jackline.

Aidha, Jackline amesema katika mchezo huo wa Stendi United dhidi ya Geita Gold, Mhandisi James Jumbe ameahidi pia kuzinunua pointi 3 kwa Sh.milioni 3 na kwamba ahadi yake ya kununua kila Goli kwa Sh.200,000 iko pale pale.

Amesema pia Mhandisi James Jumbe, awali alitoa Ofa ya kusajili wachezaji wawili kuitumikia timu hiyo ya Stendi United kuwa tayari ameshasajili wachezaji hao, na kwamba wanasubiri kukamilisha taratibu za TFF ili watangazwe rasmi.

Naye Msemaji wa Timu ya Stendi United Chama la Wana Ramadhani Zorro, amesema wachezaji wao wapo vizuri na wamejiandaa vyema kupata ushindi kwenye mchezo huo, ili kurudi na ushindi wa point 3, ambazo zina umuhimu kwao na ushindi huo utawafanya kushika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo ya Championship.

Timu ya Stendi United iliyopo katika Ligi ya Championship inashika nafasi ya 4, huku Geita Gold ikishika nafasi ya 3 kwa tofauti ya alama moja na zote zinawania kufuzu kushiriki kucheza Ligi kuu ya Tanzania Bara msimu ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *