STAMICO YAWAPA KONGOLE TAWOMA KWA KUANZISHA CHAMA, KURATIBU MAFUNZO

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limewapongeza Chama cha Wachimbaji Wanawake Tanzania kwa kuanzisha Chama cha Wachimbaji Wanawake Vijana na kuandaa mafunzo ya Usalama sehemu za kazi pamoja na utunzaji Mazingira.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini Tanzania, Dkt. Venance Mwasse wakati akifungua Mafunzo kwa wanawake wachimbaji wa madini Kahama.

“Niwapongeze sana Wanawake wa TAWOMA kwa kuanzisha hii TAWOMA youth,Hii ina maana na ustawi endelevu hawa mliowaanzisha ndiyo watakaoendeleza maono ya umoja wenu,Lakini pia niwapongeze kwa ubunifu wa mafunzo haya kwani mmewapa kitu ambacho walikuwa wanahitaji” Amesema Mwasse.

Sambamba na hayo, Dkt. Mwasse amemuomba Afisa Madini Mkoa wa Kimadini Kahama kutoa Leseni kwa kikundi cha wanawake Bugarama, ili waweze kupatiwa mashine za kuponda mawe na kujikwamua kiuchumi.

“Nikuombe afisa madini kuna ombi la hawa wanawake wa Bugarama,mimi niko tayari kuwaletea mashine za kuponda kokoto lakini wapatie leseni kwani wameamua kujikwamua kiuchumi basi tuwape nafasi na tuwasaidie katika hili,” ameongeza Mwasse.

Kwa upande wake Mratibu wa Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA), Rachel Zenno amesema kuwa faida ya kushirikisha vijana kwenye uchimbaji ni kuendelea kuvuna rasilimali madini na kuongeza kipato kwa Taifa.

“Kwa sisi vijana hii TAWOMA Youth itatusaidia kuwa halali katika sekta ya uziduaji na kuvuna rasilimali Madini hali itakayosaidia kujikwamua kiuchumi na kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema Zenno.

Kwa mujibu wa takwimu ya wachimbaji wazawa wa madini, Tanzania ina zaidi ya wachimbaji milioni sita huku wanawake wakiwa ni wengi  zaidi ya milioni tatu na laki moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *