SOKO LA MACHINJIONI MPANDA LALETA URAHISI UPATIKANAJI WA NYAMA KWA WANANCHI

Na Daniel Gahu – Katavi.

Soko la Machinjioni lililopo Kata ya Mpanda Hotel, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, limeendelea kuwa sehemu muhimu ya biashara inayowanufaisha wananchi kutokana na ratiba yake ya kipekee ya kutoa huduma kuanzia saa moja hadi saa tano asubuhi.

Tofauti na masoko mengi yanayofanya shughuli zake kwa muda mrefu zaidi, soko hili huwapa wananchi fursa ya kupata kitoweo cha nyama mapema kabla ya kuanza shughuli zao za kila siku. Hali hiyo imechangia kuongezeka kwa idadi ya wanunuzi wanaotembelea soko hilo kila siku.

Baadhi ya wananchi wanaolitumia soko hilo wanasema limekuwa msaada mkubwa kwao, hasa kutokana na upatikanaji wa nyama kwa bei nafuu na kwa wakati unaowafaa.

“Wengi wetu tunawahi kununua nyama hapa kabla ya kwenda kazini au kuendelea na shughuli nyingine. Bei zake pia ni rafiki ukilinganisha na maeneo mengine,” alisema mmoja wa wananchi aliyekutwa sokoni hapo.

Pamoja na faida hizo, wananchi wameeleza kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazohitaji kufanyiwa kazi, ikiwemo kuboreshwa kwa miundombinu ya soko ili kuongeza usafi, usalama na mazingira bora kwa wafanyabiashara pamoja na wateja.

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa husika, Ibrahim Msanda, amesema serikali imeanza kuchukua hatua za kuboresha soko hilo kwa kuweka miundombinu wezeshi itakayorahisisha shughuli za biashara na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.

Msanda amesema maboresho hayo ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha masoko yanakuwa salama, yenye mazingira mazuri na yanayokidhi mahitaji ya wafanyabiashara pamoja na wananchi wanaoyatumia kila siku.

Wananchi wameipongeza hatua hiyo wakieleza kuwa kukamilika kwa maboresho kutalifanya Soko la Machinjioni liendelee kuwa kitovu muhimu cha biashara ya nyama katika Manispaa ya Mpanda, huku likiendelea kutoa huduma bora kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo ya jirani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *