Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali itaendelea kuandaa mazingira mazuri na kuimarisha maslahi ya Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii ili waendelee kutoa huduma kwa ufanisi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika Mahafali ya Kwanza ya Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohammed Shein, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amefahamisha kuwa Serikali imejizatiti kujenga afya za wananchi ili waweze kuchangia kikamilifu katika maendeleo na ukuaji wa uchumi kupitia upatikanaji wa huduma bora za afya.
Aidha, amesema kuwa utekelezaji wa Sera ya Universal Health Coverage unalenga kutoa sura halisi ya sera hiyo kwa kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma za afya popote alipo.

Hafla hiyo iliambatana na uzinduzi wa mfumo wa M-MAMA kwa ajili ya huduma za dharura kwa mama mjamzito na mtoto kupitia matumizi ya mawasiliano kwa nambari 115, sambamba na kukabidhi vyeti kwa Wahudumu wa Afya kutoka wilaya zote.
Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru washirika wa maendeleo, taasisi za ndani na kimataifa kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kushirikiana nayo katika kuimarisha sekta ya afya nchini.

Naye Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui, amesema kuwa kupitia Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii, Zanzibar imepiga hatua muhimu ya kuwa na huduma za msingi zinazotolewa na wahudumu wenye uwezo, ikiwemo huduma za dharura.
Ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kufikia wahudumu 3,000 nchi nzima, ili kila mhudumu mmoja aweze kuhudumia kaya 500.