Na Saulo Stephen, Itigi – Singida.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, William Lupaa, amesisitiza umuhimu wa usimamizi thabiti, uwazi na kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati na thamani ya fedha inaonekana katika kila mradi.
Lupaa ametoa msisitizo huo alipokuwa akiongoza kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichoitishwa kwa ajili ya kupokea, kupitia na kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Amesema madiwani wataendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa miradi inayotekelezwa katika wilaya hiyo ili kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika ipasavyo na miradi inakamilika kwa viwango vinavyokusudiwa.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Madiwani, wataalamu kutoka idara mbalimbali za halmashauri pamoja na Kamati ya Usalama ya Wilaya, ambapo kililenga kutathmini kwa kina matumizi ya fedha na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu, afya, elimu na maji.

Katika Mjadala wa kikao hicho, madiwani walipata fursa ya kutoa maoni, kuhoji maeneo yaliyohitaji ufafanuzi na kutoa mapendekezo ya kuboresha utekelezaji wa bajeti pamoja na miradi ya maendeleo kwa kipindi kijacho.
Kikao kilihitimishwa kwa makubaliano ya kuimarisha ushirikiano kati ya madiwani na wataalamu wa halmashauri ili kuhakikisha malengo ya maendeleo ya Wilaya ya Itigi yanafikiwa kwa ufanisi na manufaa yaliyokusudiwa yanawafikia wananchi.


