SINA SHIDA NA MSHAHARA WA UBUNGE NINA SHIDA NA MAENDELEO YA MEATU – SALUM JAMBO

Na Saada Almasi, Meatu – Simiyu.

Mgombea ubunge jimbo la Meatu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salum Khamis Salum (Jambo) amewaambia wakazi wa Kijiji cha Sapa cha Kata ya Kimali Wilayani humo kuwa, dhamira yake ya kugombea nafasi hiyo ni kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kila mwana Meatu na si kusubiria mshahara ya ubunge, ili ale peke yake.

Ameyasema hayo mbele ya halaiki ya wakazi hao, waliojitokeza na kuwasihi kutofanya makosa kwa kuchagua chama pinzani, ambacho hawana uhakika wa kupata maendeleo.

“Huu uchaguzi msiuwekee ushabiki wa (Ugika na Ugalu) huo unapatikana katika (Mbina) ya siku moja lakini unapochagua unachagua kiongozi wa kukuongoza na kuleta maendeleo kwa miaka mitano,kwa hiyo ukicheza hapa tambua kuwa umechezea maendeleo yako mwenyewe,” amesema Salum.

Ameongeza kuwa uongozi ni jambo kubwa ambalo limebeba maono na matamanio ya wananchi na dhamira yake ni kuweka mbele maslahi ya wananchi kabla ya maslahi yake binafsi.

“Tambueni kuwa ninapokuwa na pambania jimbo hili sipambanii mshahara wa ubunge,tayari nina mshahara wangu kwa kazi zangu nyote mnajua, ndiyo maana kila mnapokutana na mimi huwa mnaula huo mshahara si ndivyo?!l na bado mtaendelea kula lengo langu ni kushiriki na nyie katika kuwaletea maendeleo ambayo mlinikwamisha kipindi cha nyuma mlichochagua upande mwingine,” ameongeza Salum.

Akiwa kitongoji cha Ng’hungulu Salum amemsisitiza mgombea udiwani wa kata hiyo kuhakikisha kitongoji hicho ambacho kina hadhi ya kuwa kijiji kinapata utambulisho huo ili baadae serikali ijekupeleka maendeleo ya hadhi ya kijiji badala ya kubaki kitongoji.

“Hapa Ng’hungulu tayari kuna wakazi wengi ambao wanalipa hadhi eneo hili kuwa kijiji na ilani ya chama changu niliyokabidhiwa na Mama Samia inanielekeza kuhakikisha ndani ya miaka mitano kila kijiji kipate zahanati, lakini bila kupandisha hadhi hapa zahanati haitokuja na si hivyo tu bado kuna miradi mingi inayoelekezwa vijijini hapa itapita wakati idadi ya watu ni kubwa, tunatakiwa kuwatendea haki watu hawa ili wapate huduma nzuri bora zenye utu wanaostahili,” ameongeza Salum.

Katika awamu hii Salum tayari ametikisa jukwaa la kata ya Imalaseko, Mwangudo, Bukundi na Kimali huku akitarajiwa kutikisa jukwaa la kata mama ya Mwanhuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *