SIMIYU WAJITOKEZA KUMLAKI ANAMRINGI MACHA

Na Saada Almasi – Simiyu.

Mamia ya Wananchi wa mkoa wa Simiyu wamejitokeza kumlaki Mkuu wa Mkoa mteule wa Simiyu, Anamringi Macha Wilayani Maswa akitokea mkoani Shinyanga,mapokezi yaliyoongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Prisca Kayombo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Vincent Naano

Akiongea na wananchi hao, RC Macha amemtaka kila Mwananchi atumie haki yake ya kupiga kura ifikapo mwezi Oktoba 2025.

 “Nimekuja katika mkoa huu kuwatumikia na kuendeleza pale alipoishia mwenzangu lakini niwasisitize kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba mwaka huu,ile ni haki yako ya msingi itumie,” amesema RC Macha.

Baada ya mapokezi hayo RC Macha alifika katika ofisi ya mkuu wa mkoa iliyopo mji wa kiserikali wa Nyaumata wilayani Bariadi na kupokelewa na mwenyeji wake Mhe Kenani Kihongosi ambaye ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha kwa ajili ya kumkabidhi ofisi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi Ofisi hiyo, Kihongosi amewashukuru Viongozi mbalimbali wa Serikali Mkoani Simiyu kwa ushirikiano mkubwa waliompatia katika kipindi chote alichohudumu kama Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Aidha, Kihongosi amemshukuru Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Prisca Kayombo pamoja na Sekretarieti yake kwa ushirikiano mkubwa waliompatia kipindi chote akiwa mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Naye mkuu wa mkoa mteule Anamringi Macha amesema kuwa anaupokea Mkoa huo ukiwa katika hali ya utulivu na kwamba sifa za viongozi na Watendaji wa Mkoa huo ni wachapa kazi

Aidha RC Macha amewapongeza watumishi wa mkoa huo kwa kushirikiana vyema na aliyekuwa mkuu wa Mkoa huo na kuwataka kumpatia ushirikiano zaidi ili kuendeleza kazi nzuri zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Makabidhiano ya ofisi kwa wakuu hao wawili yanafuatiwa na mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa na Rais Samia ambapo katika mabadiliko hayo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Kenani Laban Kihongosi amehamishiwa Mkoani Arusha na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuhamishiwa Mkoani humo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *