Na Saada Almasi – Simiyu.
Chama cha Wanawake Wachimbaji wa Madini Tanzania (TAWOMA), kwa kushirikiana na Shirika la Kifeminist (WOMEN FUNDS TRUST) kimetoa mafunzo wa Wanawake wanaojishughulisha na shughuli za migodi mkoani Simiyu, ili kuwapa uelewa juu ya haki zao za msingi katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Oscar Mtui ametoa pongezi kwa chama hicho ambacho kwa umoja wake wamekuwa wachangiaji wakubwa katika pato la taifa ambapo kwa mkoa wa Simiyu michango yao imepandisha makusanyo hadi kufikia asilimia 37 ya lengo la Bilioni 4 za makusanyo kwa mwaka huu ndani ya mkoa.

Amesema, “kipekee nifikishe salamu za pongezi kwenu mmekuwa wachangiaji wakubwa wa pato la taifa kwani kwa mkoa wa Simiyu kupitia tume ya madini tunakadirio la kufikisha makusanyo ya shilingi Bilioni 4 kwa mwaka ambazo hadi sasa tuko asilimia 37 ya makusanyo ambayo wanawake mmekuwa kinara wa uchangiaji huo.”
Awali akizungumza na Jambo F, Katibu wa TAWOMA, Salma Ernest amesema lengo la mafunzo hayo ni kutengeneza mazingira mazuri ya biashara miongoni mwao kwani hakuna biashara itakayo fanikiwa kwa mfanyabiashara kama hajui haki zake za msingi za biashara.

“Hii ni biashara kama biashara zingine na ili ufanikiwe katika biashara yako unatakiwa kujua haki zako za kibiashara ambazo wanawake wengi migodini hawazifahamu na kutokana na mazingira ya migodini kutokuwa na utulivu wa kutoa haya mafunzo ndiyo maana tunawaelimisha hawa ili waende kuwa mabalozi wa wenzao na kwa pamoja tuweze kukomboa jamii hii dhidi ya ukatili,” amesema Salma.
Kwa upande wake mratibu wa chama hicho, Rachel Rukwemba amesema kuwa baada mafunzo ni matarajio yao ni kuona wanawake hao wanajua haki zao za msingi kijamii,kisiasa na kiuchumi ,kutokomeza vitendo vya ukatili sambamba na kujua namna ya utunzaji wa mazingira katika maeneo yao ya kazi ili kwa pamoja waweze kuwa mfano wa kupaza sauti pale haki hizo zinapokiukwa.

“Vitendo vya ukatili maeneo ya migodi vipo ila je wanajua haki zao ili wazisemee?kwa hivyo tunatarajia wakitoka hapa wawe na uelewa juu ya haki zao za msingi ,namna ya kutokomeza ukatili dhidi yao pamoja na kuboresha mazingira kwani kinara wa mazingira ni mwanamke mara zote,” amesema Rachel
Agnes Kimoga ni mchimbaji katika mgodi wa Dutwa Wilayani Bariadi ambaye kipindi cha nyuma alishuhudia mwanamke mwenzie akitaka kufanyiwa ukatili wa kijinsia hali ambayo inamfanya awe balozi wa kukemea vitendo hivyo huku akiwataka wanawake wenzie kutofumbia macho vitendo hivyo.

Anasema, “tulikuwa tunaendelea na kazi zetu siku za nyuma ghafla tukasikia kelele za mwanamke tulisogea na kupambana na yule mtu mwovu na kufanikisha kumuokoa mwenzetu ,nawataka wanawake wote hivi siyo vitendo vya kuvifumbia macho tushirikiane kukemea.”
Hata hivyo, bado wito zaidi unatolewa kwa wanawake kujikita katika sekta ya uchimbaji nchi kwani ni kazi ambayo inaleta mafanikio kwa mwanamke, kauli ambayo imetolewa na mmoja wa wachimbaji Wilayani humo, Anisia Japhet.

“Mimi nilifundishwa na wanawake wenzangu kuwa mchimbaji na hadi leo nina miliki eneo langu na nina maisha ambayo nayaendesha kwa kazi hii pamoja na kuwapatia mahitaji yote muhimu Watoto wangu hivyo nitoe hamasa kwa wengine hii kazi inalipa usikae tu nyumbani fursa zipo,” amesema.
Malengo ya Tume ya Madini ni kukusanya kiasi cha shilingi Trilioni moja kwa migodi yote nchin, huku mkoa wa Simiyu pekee ukilenga kukusanya Bilioni 4 kwa mwaka 2025, ambazo kati ya hizo TAWOMA Simiyu kimekuwa kinara kwa kuwa wachangiaji wazuri waliofikisha asilimia 37 ya lengo mpaka sasa.