Na Gideon Gregory, Mpwapwa – Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma, George Simbachawene amesema wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuwania nafasi za Ubunge na Madiwani zinadhihirisha upendo na ukomavu wa chama hicho.
Simbachawene ameyasema hayo leo Julai Mosi, 2025 Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma mara baada ya kuchukua fomu ya kutetea kiti chake cha Ubunge katika Jimbo la Kibakwe katika ofisi kuu za CCM na kuongeza kuwa uhai wa chama chochote ni mapenzi ya watu wanapokuja kugombea.
“Uongozi wetu katika Chama Cha Mapinduzi ni wa kidemokrasia, kwahiyo chama chetu kina demokrasia pana huku chini na ndiyo maana nimeona pale wenzangu wamekuja wamechukua fomu na mimi nimechukua kwenda kuomba ridhaa ya wanachama ili watupendekeze tuweze kugombea,” amesema.

Aidha, Waziri Simbachawene amesema kuchukua fomu kujaza ni jambo moja lakini wanangojea vikao vije viwachuje na baadae vitasema anayefaa kupeperusha bendera ya CCM kwa Jimbo la Kibakwe kwani kwasasa mtihani bado ni mgumu kwasababu wagombea bado wanaendelea kuchukua fomu.
Pia, ametumia wasaha huo kuwapongeza wanachama kutoka jimboni kwake waliomchangia fedha kwa ajili ya kuchukua fomu hiyo huku wengine wakiendelea kutoa michango mbalimbali zikiwemo ng’ombe kutokana na kazi aliyoifanya katika jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kwa upande wake Mgombea mwingine katika Jimbo la Mpwapwa ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Damrkun Bi. Grace Chigongolo amerudisha fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya Ubunge katika Jimbo hilo ambapo ametoa wito kwa vijana kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika kipindi hiki.
“Vijana wenzangu tunaposikia fursa kama hizi za kuja kugombea tujitokeze tusiishie tu kwenye vitu maalum, japo si vibaya kuanzia huko kwasababu hata namimi nilianzia huko,” amesema.
Bi. Chigongolo amekabidhi fomu hiyo kwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Bw. Denise Luhende ambapo anasubilia sasa kama atapitishwa na wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM).