SIMBA YAGOMEA MCHEZO WAO NA YANGA, YATOA SABABU

Taarifa kutoka Simba SC, imeeleza kusikitishwa na vitendo visivyo vya kiungwana wakati ukiwa umebaki muda mchache kuelekea Mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Yanga SC, huku ikidai kuwa haitoshiriki mchezo huo.

Simba imeuarifu umma kuwa, kwa mujibu wa kanuni 17 (45) ya Kanuni za Ligi Kuu Bara, Timu Mgeni ina haki ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mechi katika muda tarajiwa wa mchezo husika kitu ambacho kilishindikana.

Jana usiku (Machi 7, 2025), Kikosi cha Simba SC kiliondoka katika uwanja wa Benjamin Mkapa na kurejea kambini baada ya kushindwa kufanya mazoezi ya mwisho kufuatia zuio la kuingia ndani ya uwanja linalodaiwa kutekelezwa na Makomandoo wa Yanga.

“Kwa makusudi Simba imenyimwa haki hiyo licha ya kufika uwanjani katika muda husika, katika sintofahamu hiyo, Simba iliarifiwa na Meneja wa Uwanja kuwa hana maelekezo ya kuruhusu mazoezi kufanyika bila maelekezo ya kamishna wa Mchezo, pamoja na Kamishna wa mchezo husika kufika, Mabaunsa wa Klabu ya Yanga walivamia msafara wa Simba huku wakiendelea na vurugu na wakizua Msafara wa simba kuingia uwanjani kufanya mazoezi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

“Jitihada za Simba kupata ufumbuzi wa changamoto hiyo hazikuzaa matunda kwa zaidi ya masaa mawili kabla ya Simba kuondoka eneo la nje ya uwanja kwa sababu za kiusalama ambazo zimerekodiwa kwa ajili ya ushahidi, kufuatia ukiukwaji huo wa taratibu za mchezo, Simba haitoshiriki mchezo husika na haki zote zimehifadhiwa, Simba inahimiza kuchukuliwa kwa hatua stahiki dhidi ya Wahusika wote wa sakata hili,” walimaliza Simba SC katika andiko lao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *