SIMBA DAY YAWAKUTANISHA MASHABIKI WA MUUNGANO, WARUSHA JIWE GIZANI

Na Daniel Gahu – Katavi.

Mashabiki wa Klabu ya Simba katika Kijiji cha Muungano, Kata ya Ibindi, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi, wameadhimisha kwa kishindo kilele cha Simba Day 2026, huku wakitumia siku hiyo kuonyesha mapenzi yao kwa klabu hiyo pamoja na kujenga mshikamano na amani miongoni mwa mashabiki wa soka.

Sherehe hizo zilizofanyika leo, Agosti 8, 2026, katika ukumbi wa Kijiji cha Muungano, zimekuja sambamba na maadhimisho ya miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Klabu ya Simba, huku mashabiki wakieleza matumaini makubwa kwa msimu mpya wa mashindano.

Mashabiki hao wamesema wanaamini kikosi cha Simba msimu huu kina uwezo wa kufanya vizuri katika mashindano yote itakayoshiriki na kutwaa mataji, wakieleza kuridhishwa na usajili uliofanywa na uongozi wa klabu hiyo.

Mmoja wa mashabiki kindakindaki wa Simba, Lushega Maginga, amesema usajili uliofanywa na klabu hiyo umewapa matumaini makubwa, huku akitumia nafasi hiyo kutoa utabiri wake kuelekea michezo ya watani wa jadi, Simba na Yanga.

“Msimu huu tunaamini watani zetu Klabu ya Yanga watarajie kipigo kizito na kikali cha magoli matano kwa sifuri, maana timu yetu imemsajili mshambuliaji mkali Ibrahim Doumbia kutoka Mali, yaani ni balaah. Hawa Utopolo wajipange,” amesema Maginga.

Shabiki mwingine wa Simba aliyehudhuria sherehe hizo amesema msimu huu mashabiki wa klabu hiyo wanaamini watapata matokeo makubwa dhidi ya watani wao wa jadi.

“Msimu huu tutachimba sana dawa katika ofisi za watani wetu; kwa kifupi hawatuwezi,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikundi cha Mashabiki wa Klabu ya Simba cha Kijiji cha Muungano amesema wameamua kuadhimisha Simba Day kwa lengo la kuhamasisha umoja, mshikamano na amani miongoni mwa wapenzi na mashabiki wa Simba pamoja na watani wao wa jadi, Yanga.

Amesema katika spirit hiyo, mashabiki wa Yanga nao walialikwa kushiriki katika sherehe hizo, hatua iliyolenga kuonyesha kuwa ushindani wa michezo unaweza kwenda sambamba na urafiki, upendo na amani katika jamii.

Mgeni rasmi katika sherehe hizo, Mdakuni Ramadhani Matongo, Diwani wa Kata ya Ibindi, ambaye aliwakilishwa na Mjumbe wa Chama wa kata hiyo, ameahidi kushirikiana na mashabiki hao katika kuendeleza shughuli zao.

Mgeni huyo rasmi ameahidi kujenga ofisi ambayo itatumiwa na mashabiki wa Simba katika Kijiji cha Muungano, pamoja na kusimamia mchakato wa kukisajili rasmi kikundi hicho cha mashabiki wa Simba.

Aidha, amesema ifikapo Agosti 11 mwaka huu atasafiri pamoja na kiongozi wa kikundi hicho hadi makao makuu ya Klabu ya Simba jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kufanikisha taratibu za usajili wa kikundi hicho.

Katika kilele cha sherehe hizo hakikuwa na maneno pekee, bali pia kilijawa na burudani na vyakula vya aina mbalimbali.

Mashabiki hao walisherehekea kwa kuchinja ng’ombe wawili walionona, ambapo walipata fursa ya kujumuika pamoja na kufurahia nyama choma, vinywaji pamoja na burudani mbalimbali.

Sherehe hizo ziliendelea kwa shamrashamra huku mashabiki wakionyesha furaha, upendo na mshikamano, wakisisitiza kuwa Simba Day imekuwa zaidi ya siku ya kusherehekea klabu yao; bali pia ni fursa ya kuwakutanisha watu na kuimarisha amani katika jamii.

Kwa mashabiki wa Simba wa Kijiji cha Muungano, maadhimisho ya Simba Day 2026 yameacha kumbukumbu ya aina yake, huku wakifunga siku hiyo kwa ujumbe mmoja mkubwa: mapenzi kwa Simba yanaendelea kuwaunganisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *