SIKU YA LISHE ISIMAMIWE KWA UMAKINI KUONDOKA UTAPIAMLO – DC MTATIRO

Na Eunice Kanumba –Shinyanga.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amewataka watoa huduma za afya ngazi ya jamii pamoja na watendaji wa kata kusimamia kwa umakini utekelezaji wa siku ya lishe katika vijiji, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kujenga uelewa wa wananchi na kupunguza magonjwa yatokanayo na lishe duni.

DC Mtatiro ameyazungumza hayo katika  kikao kazi cha lishe kilichowakutanisha watendaji wa kata na waganga wakuu wa halmashauri za wilaya za Shinyanga na Kishapu, ambapo ameainisha kuwa   mafanikio ya afua za lishe hayatapatikana kwa maneno pekee, bali kwa utekelezaji wa vitendo unaoonekana katika jamii.

Kikao hicho kimeandaliwa  na shirika lisilo la kiserikali la World Vision kwa lengo la kuimarisha mikakati ya lishe na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wake katika ngazi za chini.

Aidha DC Mtatiro  amesisitiza  umuhimu wa kila mshiriki kuwajibika katika nafasi yake ili kuhakikisha malengo ya kuboresha lishe yanafikiwa. Alieleza kuwa utekelezaji wa mikataba ya lishe uliyosainiwa unapaswa kuonekana kwa vitendo, hususan katika kuongeza uelewa wa familia kuhusu lishe bora na kuwahamasisha wazazi kuchangia chakula shuleni.

“Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha mikataba ya lishe inatekelezwa kikamilifu. Lengo ni kuona jamii inabadilika na kuwa na uelewa mpana kuhusu lishe, kuanzia ngazi ya familia hadi shule,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, aliwataka washiriki wa kikao hicho kuhakikisha wanatekeleza afua za lishe kwa vitendo katika maeneo yao ili kuleta matokeo ya haraka na yanayoonekana.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas Ndungile, amesema  ushirikiano kati ya World Vision na shirika la Kivulini kupitia mradi wa Grow Enrich umeanza kuzaa matunda kwa kuongeza uelewa na hamasa kwa watoa huduma za afya katika ngazi za kata na vijiji.

Alibainisha kuwa kumekuwa na mabadiliko chanya, ikiwemo kuongezeka kwa ushiriki wa wazazi katika kuchangia chakula mashuleni, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally, amekiri  kuwa pamoja na jitihada zinazoendelea, bado kuna changamoto ya mwitikio mdogo wa baadhi ya wazazi katika kuchangia chakula mashuleni, jambo linalohitaji kuendelezwa kwa juhudi za elimu na uhamasishaji.

Alisisitiza kuwa mashirika yao yataendelea kushirikiana kutoa elimu ya lishe kwa jamii, kwa lengo la kujenga kizazi chenye afya bora na chenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za utapiamlo.

Katika hatua nyingine meneja mradi wa Grow Enrich kutoka world vison Tanzania Shukran Dickson amewataka wazazi na walezi kutokuuza mazao yote waliyopata katika msimu wa kilimo uliopita ikiwemo choroko maharage na kunde badala yake wachangie mashuleni ili watoto waweze kupata chakula wanapokuwa katika masomo huku akianisha kwamba upatikanaji wa chakula mashuleni humsaidia mtoto kukua kielimu kwani anakuwa na uelewa juu ya kile ananchifundiswa na walimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *