SIKONGE YASHIRIKISHA WADAU KUZIKABILI CHANGAMOTO ZA UTORO SHULENI

Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ya mkoani Tabora, imeendelea kushirikiana na wadau wa elimu katika kukabiliana na changamoto ya utoro mashuleni, huku ikilenga kuhakikisha watoto na vijana balehe, wakiwemo wenye ulemavu, wanapata fursa ya kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao.

Hatua hiyo inatekelezwa kupitia programu inayolenga kupunguza vikwazo vinavyosababisha wanafunzi kutohudhuria masomo kwa mwendelezo. 

Programu hiyo inatekelezwa na Shirika la Restless Development katika Kata za Kisanga, Tutuo, Kitunda, Sikonge na Misheni, ikihusisha shule za msingi, sekondari pamoja na vituo vya Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Shule (IPOSA).

Katika utekelezaji wa programu hiyo, Restless Development imekabidhi vifaa mbalimbali vya kusaidia wanafunzi kuendelea na masomo, ikiwemo baiskeli, madaftari, mahindi na maharage kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Kata ya Tutuo.

Aidha, vifaa hivyo vimehusisha cherehani moja pamoja na vitambaa vilivyotolewa kwa ajili ya vikundi vya IPOSA, kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kujiajiri na kujenga msingi wa maisha yao ya baadaye.

Kwa mujibu wa mpango huo, baadhi ya changamoto zinazochangia utoro ni pamoja na ukosefu wa mahitaji muhimu ya kujifunzia na mazingira yasiyowawezesha wanafunzi kuhudhuria masomo ipasavyo. Hivyo, hatua zinazochukuliwa zinalenga kupunguza changamoto hizo na kuwawezesha watoto na vijana balehe kubaki shuleni na kuendelea na masomo yao.

Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge umesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa elimu, wazazi na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha kila mtoto anapata haki na fursa ya kupata elimu, anabaki shuleni na hatimaye kutimiza ndoto zake.

Aidha, ushirikiano huo unalenga kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanapata fursa sawa ya elimu na hawabaki nyuma katika kupata maarifa, ujuzi na fursa za kujenga maisha bora ya baadaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *