SHULE ZA SEKONDARI KALIUA ZAWEKA MISINGI KUZUIA, KUPAMBANA NA RUSHWA

Na Pascal Tuliano – Tabora.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) ni taasisi ya serikali iliyopewa jukumu la kupambana na rushwa na ni idara inayojitegemea ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais.

Tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1974 taasisi hii imekuwa na majukumu kadhaa ikiwemo kuzuia na kupambana na Rushwa katika jamii, lakini zaidi ya hayo ni kubeba jukumu la kutoa elimu kwa jamii kuanzia ngazi za shule za msingi na Sekondari ili kuwaandaa vijana wadogo kuwa na uwezo wa kukabiliana na Rushwa.

Jambo Fm imekita kambi katika Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora, lengo ni kufahamu ni kwa namna gani shule za Sekondari wilayani hapa zinawaandaa  vijana katika kukabiliana na mazingira ya rushwa.

Mwalimu Edson Bihazo ni mlezi wa Klabu ya Wapinga Rushwa katika shule ya Sekondari Kaliua, anaeleza namna wanavyowaandaa vijana hao.

“Tunawaandaa vijana kupitia majarida mbalimbali yanayotolewa na TAKUKURU lakini pia tunawaelimisha njia gani vinaweza kutumika kutoa rushwa na namna gani wanaweza kuzuia au kuzikwepa.” Amesema.

Kutoka kwa wanafunzi jambo Fm ikataka kujua wametoa wapi msukumo wa kujiunga na club hiyo ya wapinga rushwa mashuleni.

“Kilichonisukuma mimi kujiunga na PCCB Club ni kutokana na vitendo vingi vya rushwa kutokea katika jamii hadi mashuleni, sikupendezwa na hivyo vitendo kwa sababu sio halali.” Amesema Rahel Marandu, mwanafunzi wa shule ya Kaliua Sekondari.

“Kutokana na ndoto nilizojiwekea nimeamua kujiunga na club hii ya PCCB ili kujiandaa kwa maisha ya baadae maana inaniijenga nikiwa hapa.” Amesema Nelson Joseph, Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kapuya.

Mwalimu Bihazo anabainisha utaratibu waliojiwekea shuleni hapo ili kumrahisishia mwanafunzi kuripoti vitendo vya rushwa pindi anapokumbana na mazingira ya namna hiyo.

“Kama ikitokea mfanyakazi mwenzetu hapa shuleni ametenda vitendo vinavyoashiria rushwa kwa wanafunzi mara nyingi huwa wanakuja kwangu Mimi kama kiongozi wao au kwa mkuu wa shule, lakini pia tumewapatia namba za viongozi wa TAKUKURU wilaya.” Ameongeza Mwl. Bihazo.

Mkakati na misisitizo wa serikali ni kuhakikisha shule zote za msingi na Sekondari nchini zinaanzisha club ya wapinga rushwa, kama anavyoeleza mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU nchini Bwana Chrispin Chalamila.

“Natoa wito kwa shule zote za msingi na Sekondari nchini ambazo bado hazijafungua club za wapinga rushwa kuzianzisha na sisi kama TAKUKURU tutafika, ili kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wanafunzi, tukiwaelimisha na kuwahamasisha wanafunzi kuchukua rushwa tutajenga jamii imara na iliyo bora.” Amesema Chalamila.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *