Shinyanga yatekeleza vipaumbele 7  vya tume ya maendeleo ya ushirika

Mkoa wa Shinyanga umefanikiwa kutekeleza viapumbele saba vya tume ya maendeleo ya ushirika ambavyo vimewekwa na kamisheni ya tume hiyo kwa lengo la kuhakikisha ushirika unaendeshwa katika hali ya kisasa zaidi.

Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Shinyanga Bi.Hilda Boniface  amebainisha hayo wakati akizungumza katika siku ya kwanza ya jukwaa la Maendeleo ya Ushirika mkoa wa Shinyanga linalofanyika kwa siku mbili kati ya Machi 21-22 katika Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi,Taasisi ya Elimu ya  biashara Kizumbi Manispaa ya Shinyanga na kuvielezea vipaumbele hivyo kuwa ni uwekezaji katika mifumo ya kidigitali na kuwezesha usajili wa vyama 273,wakulima zaidi ya 72000,mikataba zaidi ya 40 ya vyama imepita katika mfumo huo.

Aidha amevitaja vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na kuharakisha mchakato wa uanzishwaji wa benki ya maendeleo ya ushirika,uboreshaji wa sera na sheria  za usimamizi wa vyama vya ushirika,uhamasishaji wa ushirika katika makundi maalum,uimarishaji na uthamini wa mali za vyama vya ushirika na kushirikiana na wadau mbalimbali katika uendeshaji wa sekta ya ushirika.

Akizungumza kuhusiana na ukaguzi uliofanyika kati ya Julai 2023 hadi Februari 2024 ndani ya vyama vya ushirikia katika mkoa wa Shinyanga,Mkaguzi wa vyama vya ushirika mkoa wa Shinyanga kutoka shirika la ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika Bw.Rodrick Kilemile amesema kwamba ukaguzi ulifanyika katika vyama 149 na kati ya  hivyo 46 vilipata hati safi ikiwa ni ongezeko la hati 39, 77 vilipata hati yenye mashaka 22 vikipata hati zisizo na maoni,na vyama vinne vilipata hati mbaya.

Mgeni rasmi katika jukwaa hilo ambaye ni mkurugenzi wa utafiti na mafunzo kutoka tume ya maendeleo ya ushirika Tanzania Bwana Juma Mokili Juma aliyemuwakilisha mrajis wa vyama vya Ushirika Tanzania amevitaka vyama vya ushirika kuendelea kuzingatia sheria kanuni na miongozo ya vyama vya ushirika.

Katika hatua nyingine ameupongeza uongozi wa vyama vya ushirika  mkoa wa Shinyanga  chini ya Mrajisi msaidizi kwa uandikishaji wa wanachama wengi kwa mfumo wa kidigitali wa MUVU ambapo hadi sasa wananchama wapatao 720,122 wameandikishwa na kueleza kwamba mkoa wa Shinyanga ni wa tatu kitaifa kati ya mikoa   iliyofanya vizuri katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *