SHINYANGA YAANZA MAANDALIZI USHIRIKI MAONESHO YA SABASABA 2026

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Mkoa wa Shinyanga umeanza rasmi maandalizi ya kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026, jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo imebainishwa  wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, kikiongozwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, David Lyamongi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Lyamongi amewataka wafanyabiashara wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho hayo ya kimataifa, akisisitiza umuhimu wa kujiandaa kwa bidhaa zenye ubora zitakazoweza kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.

Amesema ushiriki wa Mkoa wa Shinyanga katika maonesho ya Sabasaba mwaka 2025 ulizaa matokeo chanya, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa utambuzi wa bidhaa zinazozalishwa mkoani humo, hususan mchele ambao umeanza kujipatia sifa kwa ubora wake kitaifa.

“Tunapaswa kutumia fursa hii vizuri zaidi mwaka huu kwa kuhakikisha tunapeleka bidhaa bora zitakazoiwakilisha vyema Shinyanga na kuvutia masoko mapya,” amesema Lyamongi.

Ameongeza kuwa maonesho ya Sabasaba ni jukwaa muhimu la kibiashara linalokutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo kutoa nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa wafanyabiashara na mkoa kwa ujumla.

Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki kikao hicho wamesema wamejipanga kuongeza ubora wa bidhaa zao ili kuhakikisha wanaitangaza vyema Shinyanga katika maonesho hayo.

Wamesisitiza kuwa mwaka huu wataweka mkazo zaidi katika ubunifu, ufungashaji na ubora wa bidhaa ili kuvutia wateja na masoko mapya ya kimataifa. 

Kikao hicho pia kimeazimia kuongeza hamasa kwa wafanyabiashara wengi zaidi kushiriki, pamoja na kuhakikisha kuwa Mkoa wa Shinyanga unakuwa miongoni mwa washiriki wanaojitokeza kwa ubora na utofauti katika maonesho hayo.

Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa moja ya jukwaa kubwa la kibiashara   nchini Tanzania, yakitoa fursa kwa wazalishaji na wafanyabiashara kujitangaza, kujifunza na kupanua mitandao ya kibiashara katika soko la kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *