Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Ikiwa Juni 28 ni siku ya mwisho kwa Madaktari Bingwa wa Samia kutoa huduma za afya za kibingwa wanakamilisha kazi hiyo katika mkoa wa Shinyanga, baadhi ya Wananchi mkoani humo wameomba kama kuna uwezekano wa kuongezwa siku, ili changamoto za Afya zinazowakabili ziweze kutatuliwa kutokana na mahitaji kuwa bado ni makubwa.
Wananchi hao, wamebainisha hayo wakati wakizungumza na Jambo fm ilipofika katika hospital ya manispaa ya Shinyanga, ili kujionea huduma hizo zinavyoendelea kabla ya kutamatishwa hapo kesho na kukuta kundi kubwa la watu wakisubiri kupatiwa huduma.

“Hatujui kwa wingi wetu huu kama kweli hizi siku sita zilizopangwa kama zitatutosha kama unavyoweza kuona Umati huu wa watu waliokuja kupata huduma za kibingwa,” amesema Mzee John Mandu mkazi wa Chamaguha mkoani Shinyanga.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Manispaa, Dkt. Moshi Ryioba amesema kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu ikilinganishwa na siku zingine ambazo.

“Tumepokea wananchi wengi kwani kwa siku tumekuwa tukihudumia wananchi 160, za Zaidi hii sio hali ya kawaida kwani idadi ya kawaida huwa ni watu kati ya 50 hadi 70 kwa siku za kawaida,” amesema Dkt. Ryioba.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Boazi Mwasambili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, amekiri kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wenyeji wake na kufanikisha Operesheni mbili huku akijiandaa kufanya zingine nne (4).

“Kama unavyoweza kuona hapa nipo na wataalam wawili, ambao tumekuwa nao bega kwa bega tangu siku ya kwanza kuna siku tulitoka hapa karibu saa mbili za usiku lakini hawajaacha kunipatia ushirikiano wakutosha,” amesema Dkt. Mwasambili.
Madaktari Bingwa walioweka kambi katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga ni pamoja na Daktari bingwa Watoto, Wanawake, Upasuaji, Pua, Koo na Sikio,Magonjwa ya ndani, Meno pamoja na Wauguzi Mabingwa.