SHINYANGA: WACHIMBAJI WASITISHA SHUGHULI KUSUBIRI MUAFAKA WA TOZO

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Wachimbaji wadogo wa madini katika Mgodi wa Mwakitolyo, uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wamesitisha shughuli za uzalishaji, wakisubiri uamuzi wa kamati iliyoundwa kushughulikia malalamiko yao kuhusu tozo mpya ya Shilingi 200,000 kwa kila gari linalotoka mgodini likiwa na mawe.

Hatua hiyo imechangiwa na kuanzishwa kwa tozo  hiyo kwa kila gari linalobeba mawe kutoka mgodini, jambo ambalo wachimbaji wanasema ni kubwa  hailingani na hali halisi ya uzalishaji na gharama za uendeshaji.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wilaya ya Shinyanga, Leonard Waziri.

Akizungumzia suala hilo Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wilaya ya Shinyanga, Leonard Waziri amesema, kusimama kwa uchimbaji kumeathiri si wachimbaji pekee bali pia shughuli nyingine za kiuchumi zinazotegemea sekta hiyo katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa ni muhimu serikali kushughulikia kwa haraka suala hilo ili kupunguza mzigo wa tozo na kurejesha mzunguko wa uchumi kwa wachimbaji na jamii inayowazunguka.

Janeth Ngangula.

Mchimbaji mdogo wa madini, David Elias, amesema kusimama kwa uzalishaji kumezidisha hali ngumu ya kiuchumi kwa wachimbaji na kuomba serikali kuharakisha suluhisho ili kurejesha shughuli hizo muhimu.

Kwa upande wake, Janeth Ngangula amesema wachimbaji wako tayari kulipa tozo, lakini kiwango kilichowekwa ni kikubwa mno, na kusisitiza kuwa kamati iliyoundwa inapaswa kuharakisha mchakato wa kupitia upya tozo hiyo.

Frank Moshi.

Naye Frank Moshi, amependekeza kiwango hicho kipunguzwe hadi kufilika shilingi elfu ishirini  kwa kila gari, akieleza kuwa kiwango hicho kinaweza kuendana na uhalisia wa uzalishaji na kuwapa wachimbaji nafasi ya kuendelea na shughuli zao.

 Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, alikutana na wachimbaji hao na kusikiliza malalamiko yao kabla ya kuunda kamati iliyojumuisha pande zote mbili wachimbaji na watalaam kutoka Halmashauri  ili kupitia upya tozo hiyo na kufikia muafaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *