SHINYANGA NI SALAMA UCHAGUZI UTAKUWA WA AMANI – POLISI

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, limewahakikishia Wananchi wa Mkoa huo kuwa kutakuwepo amani siku ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025 na kuwataka wajitokeze kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura ili, kuwachagua viongozi wanaowataka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi ametoa kauli hiyo hii leo Oktoba 18, 2025 wakati akizungumza na Madereva wa Bajaji, Bodaboda na Magari madogo (haice) katika Soko Kuu la Mjini Shinyanga.

Amesema, Jeshi hilo lipo kamili kulinda Amani siku ya Uchaguzi Mkuu, na kwamba wananchi wasiwe na wasiwasi, bali wajitokeze kwa wingi kupiga kura, na kutumia haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi wanaowataka ambao watawaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga tumejipanga vyema kuhakikisha amani inaendelea kutawala siku zote na siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29,tunawaomba wananchi wote wajitokeze kwenda kupiga kura sababu amani itakuwepo na hakutakuwa na vurugu zozote,” amesema Magomi.

Aidha, amewaonya watu au baadhi ya vikundi kama wapo ambao wamepanga kufanya vurugu siku ya uchaguzi, kwamba wasije kuthubutu, sababu wamejipanga vyema kudhibiti fujo na kusisitiza jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yao.

Naye Mwenyekiti wa Boda Boda Manispaa ya Shinyanga, Juma Mrabu amesema vijana wa bodaboda hawapo tayari kutumika kuvuruga amani ya nchi siku ya Uchaguzi Mkuu, bali watashiriki kwenda kupiga kura na kurudi kuendelea na shughuli zao kama kawaida za kujitafutia kipato.

Oktoba 29 ni siku ya kupiga kura ya kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani ambao wataongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo hadi 2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *