Na Saada Almasi, Meatu – Simiyu.
Mgombea nafasi ya ubunge wa Jimbo la Meatu kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salum Khamis Salum (Jambo) amewahakikishia wananchi kuwa amejidhatiti na kulivalia njuga tatizo la ukosefu wa maji safi na salama ambalo kwa sasa limeota mizizi,kuleta adha kwa wananchi wa maeneo hayo na kugeuka kuwa kati ya vikwazo vya maendeleo ya jimbo hilo.
Salum ameyasema hayo kwa nyakati tofauti pindi akizinadi sera za chama chake kwa wananchi wa baadhi ya vijiji vilivyo katika kata 16 zinazounda jimbo hilo na kusisitiza kwamba ilani ambayo amepewa na chama cha Mapinduzi imebeba miradi ya kimaendeleo zaidi ya 70 ambayo kati yake kuna mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Victoria ambao ukamilifu wake unakwenda kuwa suluhu ya kudumu ya shida ya maji wanayopitia wakazi hao.
“CCM imenipatia ilani ambayo imesheheni miradi zaidi ya 70 ya kimaendeleo ukiwemo mradi wa Ziwa Victoria unaotekelezwa kwa shilingi Bilioni 440,lakini mradi huu awaliuliwekwa awamu ya pili ili kutufikia hapa Meatu na ukiangalia asili ya jimbo letu ni kame zaidi kuliko wilaya zote mkoani Simiyu,”

“Kutokana na hilo nimefanikiwa kunong’ona na Mama Samia atusogezee mradi awamu ya kwanza kwa kumpa sababu zenye mashiko na ushawishi na amenielewa katuweka awamu ya kwanza kwa kuwa dhamira yake pia ni kumtua mwanamke ndoo kichwani,” amesema Salum.
“Na mradi huu utakapotufikia kila utakapopita wakazi wote waishio kilometa 12.5 kutoka eneo lilipolazwa bomba watapata maji ndiyo maana nasema wote mtafikiwa na mradi huu kwa sababu maeneo mengi yaliyokaribu na mradi yapo ndani ya umbali huo,” ameongeza Salum.
Amesema kuwa katika kusubiria kufikiwa na mradi huo ambao unaanzia wilayani Busega kisha Bariadi,Itilima hadi Meatu kutafanyika jitihada za makusudi za kutafuta vyanzo vya maji vipya vitakavyokwenda sambamba na uchimbaji wa visima ili wananchi waendelee kupata huduma hadi pale mradi utakapowafikia.

Aidha Salum Jambo ameeleza kuwa ilani pia imetaja umaliziaji wa “magofu” ya zahanati ,vyumba vya madarasa na hata nyumba za walimu katika maeneo yote ambayo hayakukamilika ili wananchi wawe na uhakika zaidi wa kupata huduma bora
” ndani ya ilani hii pia imetaja magofu sasa mimi Jambo ninasema magofu ni marufuku labda yawe mapya mtqkayojenga leo,kila ninakopita kuna vyumba vya madarasa ,nyumba za walimu,ambazo katika kipindi changu nilianza kujenga baadae mlipokengeuka na kumchagua mwingine miradi ikasimama sasa mwenye miradi nimekuja mtasahau kuhusu magofu,” Salum Jambo.
Akimwombea kura Mama Samia ya kupewa nafasi ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Salum amesema kuwa licha ya fedha nyingi ambazo Mama Samia ameahidi kuzitoa za kimaendeleo jimboni humo bado kuna ajira kwa watumishi ambazo zitatolewa ndani ya siku 100 za mwanzo akiwa madarakani.

“Mna kila sababubu ya kumpa kura za ndio Mama Samia kwani ameahidi kutoa ajira zaidi ndani ya siku 100 akiwa madarakani na bado kuna madarasa 120 ambayo ametupatia katika jimbo hili ambayo yanaambatana na uchimbaji wa matundu ya vyoo vya wanafunzi pamoja na ujenzi wa zahanati,” amesema Salum.
Salum pia amezungumzia agenda vipaumbele vya jimbo hilo ambazo ni ujenzi na ukarabadi wa barabara,maboresho ya kilimo cha mkataba katika zao la pamba ambacho hakikuwa na ushindani pamoja na mapambano yake dhidi ya wanyama tembo ambao wamekuwa na desturi ya kuvamia makazi ya watu na kuharibu mali zao.


