Na Saada Almasi – Simiyu.
Mzee mmoja, Njole Nhanda Mbuluzi (71), mkazi wa mtaa wa Nyamimbi kata ya Somanda mjini Bariadi, ameaga dunia baada ya kushambuliwa na Nyuki waliokuwa wameweka makazi karibu na nyumba anayoishi.
Mzee huyo mwenye ulemavu wa miguu amekutwa na madhila hayo baada ya mtoto wa jirani kufika katika eneo ulipo mti huowenye Nyuki na kuanza kuwarushia mawe licha ya kwamba alimkataza mara kadhaa bila mafanikio.
Kazi Njole mtoto wa mzee huyo anasema kuwa yeye ndiye aliyekuwa nyumbani na baba yake wakati nduguze wengine wakienda matembezi na muda mchache tu alipoondoka kwenda dukani akimuacha baba yake ndipo tukio hilo lilipomkuta.
“Nimekaa na baba hadi mida ya saa kumi jioni nikatoka mara moja kwenda dukani lakini sasa kabla sijafika nikasikia yowe kutoka kwetu nikaja mbio kufika namkuta baba amezingirwa na nyuki nikachukua maji kuanza mumwagia lakini haikusaidia kitu,” amesema Kazi.
Kutokana na hali aliyokuwa nayo mzee huyo ya kujeruhiwa kila mahali na nyuki mmoja wa vijana wake Emmanuel Njole ambaye pia alifika eneo hilo na kufanikiwa kuwajulisha jeshi la zimamoto na uokoaji ili kusaidia kuokoa maisha ya baba yake
“Sikuwa na njia yoyote ya kumsaidia maana nyuki walijaa usoni mwilini kila mahali ikabidi nipige simu jeshi la zimamoto ndio wakawahi kuja kumchukua na kumpeleka hospitali lakini hakukaa sana akafariki maana sumu ilikuwa imeenea mwili mzima,” amesema Emmanuel
Mwenyekiti wa mtaa huo, Juma Mashauri amethibitisha kuondokewa na mzee huyo na kutoa onyo kali kwa watu wanaopenda kuchokoza nyuki wanaojiweka katika maeneo yao ya karibu
Amesema, “mimi nilipigiwa simu na nikafika wakati tayari jeshi la zimamoto wanamchukua na kumkimbiza hospitali,lakini wale nyuki walikuwa pale siku zote wasinge chokozwa wasingedhuru mtu,nakemea watu wenye hizo tabia” amesema Juma
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoani Simiyu, Faustine Mtitu ametoa angalizo kwa wananchi kutoa taarifa kwa vyombo husika za uwepo wa nyuki karibu na makazi yao ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika
“Nitoe wito kwa wananchi wote kama umekaa sehemu kuna viashiria vya uwepo wa nyuki kwanza toa taarifa,pili usiwachokoze kwa namna yoyote na mwisho kama ni eneo lako la kazi za kiuchumi mfano kilimo nakutaka uache mara moja hadi mamlaka itakapofika na kuwaondoa mahali hapo,” amesema Mtitu