SHABAN AFUNGWA MIAKA 30 JELA KWA KUBAKA MWANAFUNZI.

Shaban Lyahasi (24), mkazi wa Kijiji cha Mwanekeyi, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 15, ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kisheria.

Hukumu hiyo imetolewa katika Mahakama ya Wilaya ya Kwimba na Hakimu Mwandamizi, John Chai Jagadi, mbele ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Juma Kiparo. Kesi namba 26610/2024.

Inadaiwa kuwa tukio hilo lilitokea tarehe 5 Septemba 2024, katika Kijiji cha Mwamanga, ambapo Lyahasi alimbaka binti huyo ndani ya chumba chake, akimuahidi kuwa atamuoa. Hii ni kinyume na kifungu 130(1)(2)(e) na 131(1) vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria Marejeo ya Mwaka 2022.

Lyahasi alifikishwa mahakamani tarehe 18 Septemba 2024, ambapo alikana kutenda kosa hilo. Hata hivyo, mwendesha mashtaka alileta mashahidi wanne, akiwemo mwathiriwa, na baada ya kusikiliza ushahidi, Hakimu Jagadi aliona kuwa mshtakiwa alikuwa na kesi ya kujibu. 

Katika hatua ya kujitetea, Lyahasi alishindwa kujizuia na kuangua kilio, lakini kilio hicho hakikusaidia kuondoa hatia. Mwendesha mashtaka alisisitiza umuhimu wa kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa, akieleza kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake vinakwamisha juhudi za serikali za kuwasaidia watoto wa kike kumaliza masomo yao.

Hakimu Jagadi amemhukumu Lyahasi kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na pia aliamuru alipe fidia ya shilingi laki tatu kwa binti aliyetendewa ukatili huo. Hukumu hii inatoa ujumbe mzito kuhusu umuhimu wa kulinda haki za watoto na wanawake katika jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *