Na Melkizedeck Anthon – Mwanza.
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kukamilika kwa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kutarahisisha usafiri, kuongeza ufanisi wa biashara na kupunguza mfumuko wa bei unaochochewa na gharama kubwa za usafirishaji wa bidhaa.
Akizungumza leo Jumatano, Oktoba 8, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza, Dkt. Samia amesema serikali inaendelea na ujenzi wa kipande cha reli cha Mwanza–Isaka chenye urefu wa kilomita 314, kinachogharimu takribani shilingi trilioni 3 na hadi sasa kimefikia asilimia 63 ya utekelezaji.
Amesema kupitia mradi huo, Mkoa wa Mwanza utakuwa na vituo vitatu vya kushusha na kupakia abiria katika maeneo ya Mwanza Mjini, Fela, Mantare, Bukimbwa na Malya, huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kuwekeza kwenye vitega uchumi kama hoteli, migahawa na nyumba za kulala wageni pembezoni mwa vituo hivyo.

“Tutakapomaliza na kuunganisha Dar es Salaam hadi Mwanza, safari itapungua kutoka saa 18 hadi saa nane pekee. Hii itarahisisha biashara, mzigo utakaosafirishwa Dar es Salaam utawasili Mwanza siku hiyo hiyo,” alisema Dkt. Samia.
Amefafanua kuwa kukamilika kwa reli hiyo kutasaidia kushusha gharama za usafirishaji, jambo litakalopunguza bei za bidhaa sokoni na hatimaye kupunguza mfumuko wa bei kwa wananchi.
“Gharama za kusafirisha bidhaa zikishuka, bei sokoni pia zitapungua kwa sababu bei ya bidhaa inaendana na gharama ya usafirishaji,” alisema.

Aidha, Dkt. Samia amebainisha kuwa serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama reli, barabara na bandari ili kuimarisha miundombinu ya usafiri, kuongeza biashara na kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na maendeleo hayo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samia amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake kupitia serikali ya awamu ya sita, Mkoa wa Mwanza umenufaika na zaidi ya shilingi trilioni 5.6 zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo – kiwango ambacho hakijawahi kutolewa kwa mkoa mmoja nchini.
Fedha hizo, amesema, zimetumika kuboresha huduma za afya, kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga, pamoja na kupunguza rufaa za wagonjwa kuelekea Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa hospitali kubwa mbili za rufaa mkoani humo, Sekou-Toure na Bugando, zimeboreshwa kupitia miradi mikubwa ya ujenzi na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa ikiwemo mashine mbili za CT-Scan, na mtambo wa kuzalisha hewa ya oksijeni.
Dkt. Samia amesema katika Hospitali ya Sekou-Toure serikali imejenga jengo la mama na mtoto lenye ghorofa tano kwa gharama ya shilingi bilioni 10.1, lenye uwezo wa kuhudumia vitanda 261 kwa wakati mmoja, jambo lililopunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya uzazi.
Kwa upande wa Hospitali ya Bugando, ameeleza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 9 zimetumika kuboresha huduma, kununua vifaa tiba, kujenga wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) na jengo jipya la matibabu ya saratani, pamoja na mashine maalum za uchunguzi na mionzi ya saratani ya matiti.

“Tunataka huduma zote za kibingwa zipatikane hapa Mwanza ili tupunguze rufaa za wagonjwa kwenda Dar es Salaam na kwingineko,” alisisitiza Dkt. Samia.
Aidha, amebainisha kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuunda serikali katika uchaguzi ujao, atazielekeza jitihada zaidi katika Kisiwa cha Ukerewe kwa kuboresha Hospitali ya Nansio, kujenga majengo ya dharura na kuanzisha hospitali ya kibingwa kwa ajili ya wakazi wa kisiwa hicho.


