
Na Saada Almasi – Simiyu
Serikali imetoa shilingi bilioni 23 milioni 980 katika kuboresha elimu ya msingi na sekondari wilayani Meatu mkoani Simiyu zikiwemo shilingi bilioni 8 milioni 640 kwa ajili ya elimu bila malipo uwekezaji ambao umeongeza idadi ya wanafunzi wa sekondari kutoka 9484 mwaka 2022 hadi kufikia 12682 mwaka 2025
Hayo yamesemwa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya ya Meatu katika ziara yake ya siku tano mkoani Simiyu akisema kuwa ongezeko hilo limetokana na maboresho na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu
“Huu uwekezaji tuliouweka na umeongeza idadi ya wanafunzi wanaojitokeza kupata elimu kwa kuwa sasa hivi mazingira ya kusoma ni mazuri na hata idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kwa ajili ya elimu ya awali kufikia 9569 bila mchango wowote kutoka kwa mzazi”amesema Rais Samia
Ameongeza kuwa katika kumwezesha mwananchi kiuchumi jumla ya shilingi milioni 769 zimetolewa katika vikundi 89 vya vijana akina mama na watu wenye ulemavu kama mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri tangu mwaka 2021
“Fedha hizi kwa ajili ya mikopo kwa makundi haya zimekwenda kuwawezesha vijana,akina mama na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi,na nichukue nafasi hii kuzipongeza halmashauri zote nchini kwa kusimamia zoezi la utoaji wa mikopo hiyo” ameongeza Samia
Aidha amewataka wafugaji wilayani humo kuendelea kutumia kituo cha uwakala wa maabara ya wanyama kiliyojengwa wilayani humo ili kuweza kupima na kubaini magonjwa ya mifugo na hatimaye kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo