Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, amesema kuwa utekaji wa Mtanzania huko nchini Nigeria ni viashiria vya ugaidi. Dk Tax ameyasema hayo jijini Arusha, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara ya kutembelea miradi ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

“Ni kweli kuna Mtanzania mwenzetu ametekwa huko Nigeria na tunatoa pole kwa familia yake na Kanisa Katoliki nchini, na ili linatokana na matatizo ya kiusalama katika nchi na ugaidi,” amesema waziri huyo mwenye dhamana ya mambo ya nje. Amesema kuwa hadi sasa hakuna sababu ya msingi iliyotolewa na watekaji hao, zaidi ya kudai pesa ili kuwaachia.
Mtanzania huyo Melkiori Mahinini (27) ambaye ni frateri wa Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers) mzaliwa wa Parokia ya Kabanga, Jimbo la Kigoma, alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Agosti 3 mwaka huu, katika jimbo la Minna huko Nigeria akiwa na mwenzake, Padri Paul Sanogo, raia wa Burkina Faso. Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana amesema Serikali kwa kushirikiana na taasisi husika wanachukua hatua mbalimbali kuhakikisha Mtanzania huyo, pamoja na mwenzake wa Burkina Faso wanaachiwa huru.