SERIKALI YATENGA BILIONI 100 KILA MWEZI KULIPA MADENI YA WAKANDARASI

Na Daniel Gahu – Katavi.

Serikali imetangaza mpango wa kutenga Shilingi bilioni 100 kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara nchini, hatua inayolenga kuongeza kasi ya utekelezaji na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani Katavi, akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha miradi yote ya barabara inayoendelea nchini inakamilika kwa kutoa fedha kwa wakati.

“Serikali imeahidi kulipa bilioni 100 kila mwezi ili kulipa wakandarasi wanaoendelea na ujenzi wa barabara nchini ili miradi hiyo ikamilike,” amesema Ulega.

Waziri huyo amesema kwa sasa Serikali haitaanzisha miradi mipya ya barabara, bali itaelekeza nguvu na rasilimali zake katika kuhakikisha miradi ambayo tayari imeanza inakamilika.

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Kibaoni–Sitalike yenye urefu wa kilomita 70, Ulega amesema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na mchango mkubwa katika kuchochea shughuli za kiuchumi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na kuimarisha mahusiano ya kibiashara na nchi jirani.

Amesema barabara hiyo itarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko pamoja na kufungua fursa mpya za biashara kwa wananchi wa Katavi na mikoa jirani.

“Serikali itaendelea kuhakikisha inatenga na kutoa fedha kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huu kukamilika kwa mujibu wa viwango na muda uliokusudiwa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amesema Serikali tayari imelipa Shilingi bilioni nne kwa ajili ya ujenzi wa Barabara inayoanzia Vikonge (Tanganyika) kuelekea mkoani Kigoma.

Ameagiza mkandarasi kuongeza kasi ya kazi, hususan kukamilisha ujenzi wa Daraja la Mnyamasi, ili kurahisisha matumizi ya barabara hiyo na kuondoa changamoto za mawasiliano zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.

Ulega pia amewataka wasimamizi wa miradi kuhakikisha maeneo yote yanayokatisha mawasiliano wakati wa mvua yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji bila kuathiri ubora wa miundombinu.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega.

Akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi ya Mkoa, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi, Eng. Martin Mwakabende, amesema ujenzi wa kipande cha kwanza cha Barabara ya Kibaoni–Sitalike umegawanywa katika sehemu tatu.

Amesema gharama ya ujenzi wa kipande hicho inafikia Shilingi bilioni 88.72.

Ujenzi wa Barabara ya Kibaoni–Sitalike ni miongoni mwa miradi inayolenga kuimarisha mtandao wa barabara nchini, kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayounganishwa na barabara hiyo.

Kwa ujumla, mpango wa Serikali wa kutenga Shilingi bilioni 100 kila mwezi kwa ajili ya kulipa wakandarasi unatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya barabara na kusaidia kukamilisha miradi ambayo imekuwa ikiendelea nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *