Na Adam Msafiri – Musoma.
Serikali wilayani Musoma mkoani Mara imeutaka uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kuhakikisha Watendaji katika idara mbalimbali wanatoa huduma bora na stahiki kwa wananchi, hatua inayolenga kupunguza na hatimaye kumaliza migogoro inayotokana na ucheleweshaji au ukosefu wa huduma.
Hatua hiyo imekuja sambamba na kuendelezwa kwa mpango wa kambi jumuishi za utoaji huduma, unaolenga kusogeza huduma karibu zaidi na makazi ya wananchi ili kuongeza upatikanaji wake kwa urahisi.

Akizindua awamu ya pili ya kambi hizo katika eneo la Bweri mjini Musoma, Mkuu wa Wilaya hiyo Juma Chikoka, amewataka watendaji wa umma kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha kila mwananchi anayefika kambini anapata huduma inayostahili kwa wakati.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Nyabiti pamoja na Diwani wa Kata ya Bweri, wamesema kambi hizo ni suluhisho muhimu kwa changamoto za upatikanaji wa huduma, hasa kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni ambao hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Wananchi nao wameipongeza serikali kwa jitihada hizo, wakisema zimepunguza usumbufu na gharama walizokuwa wakizitumia hapo awali kufuata huduma mbali na makazi yao,baadhi yao wamesema uwepo wa kambi hizo unarahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wakati na kuongeza ufanisi katika kushughulikia changamoto zao.


