Katika kupambana na tatizo la gugu maji katika Ziwa Viktoria, Serikali imesema tayari mtambo mmoja wa kuondoa magugumaji umepatikana huku jitihada za kununua mitambo mingine zikifanyika ili kuondoa adha kwa watumiaji wa ziwa hilo.
Akizungumzia ujio wa mtambo huo, Katibu Mkuu ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema ujuo wa mtambo huo utakuwa msaada mkubwa wa kupambana na gugu maji hilo ambalo tayari lilikua limeanza kuwaathiri wananchi wanaofanya shughuli zao kupitia ziwa hilo.

“Kwa mtambo huu wa kwanza na mingine ipo njiani inakuja, changamoto hii kwa kiasi fulani tutakwenda kuikabili na nipende kumshukuru Waziri Mkuu kwa maelekezo yake na kwa sasa kazi inakwenda vizuri,” alisema Mhandisi Luhemeja.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Luhemeja amesema kwa siku za hivi karibuni gugu maji hilo limekuwa ni changamoto kubwa na limekuwa likiathiri shughuli nyingi zinazofanyika katika Ziwa Viktoria, ikiwemo shughuli za uvuvi pamoja na shughuli nyingine.

“Magugumaji ni changamoto kubwa kwa sababu yanaathiri pia usafiri na yanathiri uchumi kwa sababu samaki wanafukuzwa na wanakosa oksijeni ya kutosha.”
Kwa upande wake Fundi Mwandamizi wa mtambo huo Dankani Mgata amesema tayari mtambo huo umeanza kufanya kazi ya kutoa magugumaji katika ziwa hilo na una uwezo wa kuchimba kina cha chini cha maji mita saba huku pia ikiwa na uwezo wa kuondoa gugu maji heka moja kwa siku.

Hata hivyo Serikali imesema ina mipango ya kuendelea kuongeza mitambo mingine ili kuhakikisha tatizo la gugu maji linashughulikiwa kwa ufanisi zaidi huku malengo mengine ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na jinsi gugu maji linavyoweza kudhibitiwa.