Na Irene Kishiwa – Chumba cha Habari.
Wananchi Mkoani Shinyanga, wameipongeza Serikali kwa kupiga marufuku matumizi ya watoto hususan wa kiume, kuhudhuria katika sherehe na burudani zinazochochea vitendo vya mmomonyoko wa maadili na zinazokuwa kinyume na mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.
Kwa nyakati tofauti, Wananchi hao wamesema vitendo hivyo ni sawa na ukatili unaofanywa dhidi ya kundi la Watoto, ambao ni tegemeo kwa familia zao na Taifa kwa ujumla katika siku zijazo, na kwamba matumizi yasiyo sahihi kwa watoto wa kiume katika sherehe yanauondoa utu.
Katika hatua nyingine wameiomba Serikali kuchukua hatua za kisheria, dhidi ya mtu ama kundi la watu ambao wanajihusisha na vitendo hivyo, ili iwe fundisho na pia kulinda utu na nafasi yao katika jamii.

“Tunafahamu na tunaipongeza Serikali kwa hatua hiyo na tunafahamu kuwa ina mkono mrefu hivyo haitasita kuwachukulia hatua kali na kuwatafuta popote waliopo waandaaji na wanaohusika kutafuta Watoto hao wakidhani wanapamba sherehe zao kumbe wanawadhalilisha bila ya Watoto hao kujua kama wanatumiwa ndivyo sivyo,” walisema.
Hivi karibuni, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum dokta Dorothy Gwajima alitoa katazo hilo katika taarifa yake kwa umma Agost 16 mwaka huu ikieleza katazo hilo lililowataka waandaaji wa sherehe na burudani za aina hiyo kujisalimisha katika kituo cha Polisi kilicho karibu nao ifikapo Agosti 19, 2026.

Alisema, endapo wahusika hawata tekeleza agizo hilo atamwomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuwezesha Jeshi la Polisi kufanya msako mahsusi kwa kushirikiana na jamii, ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Aidha, aliwataka Maafisa Utamaduni pamoja na Watendaji wa Serikali za Mitaa na Vijiji kuongeza umakini katika uchambuzi wa maombi ya vibali vya sherehe na burudani, ili kubaini mapema viashiria vya shughuli zinazoweza kukiuka maadili na kutupilia mbali maombi yenye mashaka.


