Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema katika robo ya kwanza ya mwaka 2023/2024, mapato kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje yalifikia Shilingi Trilioni 9.06 sawa na Asilimia 89.6 ya lengo la kipindi hicho.

Amesema hayo leo (Ijumaa, Novemba 10, 2023) wakati akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Januari 30, 2024.
Amesema kuwa ongezeko hilo ambalo limewezesha Taifa kuimarika kiuchumi limetokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita ikiwemo kuwezesha uwekezaji wa kimkakati katika sekta za uzalishaji, huduma za jamii na miundombinu.
Majaliwa amesema kuongezeka kwa mapato hayo, kunatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kurahisisha ulipaji wa kodi.
Katika hatua nyingine, Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) iboreshe mwongozo wa uwekezaji ili kubainisha fursa kulingana na mazingira ya sasa na kuzingatia taratibu za kuwatambua na kuwasajili wanaotaka kuwekeza nchini.