
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kwa sasa Serikali imejikita katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vitakavyotumika katika Mashindano ya AFCON 2027.
Waziri Ndumbaro ameyasema hayo leo Aprili 16,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Tarime Mjini Mhe. Michael Mwita Kembaki aliyetaka kujua ni Serikali ina mkakati gani wa Kujenga uwanja wa Michezo Wilaya ya Tarime.
Amesema Viwanja hivyo ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa Arusha na Dodoma na ukarabati Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru vilivyopo Jijini Dar es Salaam na kuongeza kwamba Serikali ipo tayari wakati wowote kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wamiliki na wadau mbalimbali wa michezo wanaokusudia kujenga au kuboresha miundombinu ya michezo kwa kuzingatia miongozo ya mashirikisho ya michezo husika ukiwemo uwanja wa Tarime, kama inavyoelekezwa na kifungu cha 7 (i) –(ii) na (iv) cha Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995.