
NA EUNICE KANUMBA-SHINYANGA
Matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kutumia Ndege Nyuki (Drone) kunyunyizia dawa za kuuwa wadudu kwenye zao la pamba imeondoa adha kwa wakulima kutumia muda mrefu kufanya kazi hiyo.
Hayo yamebainishwa na wakulima wa zao la pamba katika Kijiji cha Kinampanda na Mwamalasa Katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha ya kukagua maendeleo ya zao hilo na kusisitiza umuhimu wa kunyunyizia dawa za kuuwa wadudu.
Ngusa Mayunga mkulima katika Kijiji cha Mwamalasa Wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga,amesema amelima ekari kumi chini ya usimamizi wa wataalamu wa kilimo nakufuata kanuni bora ya ulimaji wa zao hilo kwa kuepuka kuchanganya na mazao mengine ili kuwa na mafanikio makubwa.

Mayunga amesema kipindi hiki nichakunyunyuzia dawa na kwamba amekuwa akitumia pampu kwa kuibeba mgongoni wakati mwingine anachoka nakutumia muda wa siku mbili au tatu kukamilisha shamba ekari moja ambapo kwa ndege nyuki inatumia dakika sita kwa ekari.
Mkulima mwingine Muhoja Peter mkazi wa Kijiji cha Kinampanda, amesema kunyunyizia dawa ya kuuwa wadudu kwenye pamba kwa kutumia pampu ya mkono ni changamoto kubwa kwani wanatumia nguvu kubwa ambapo kwa sasa uwepo wa ndege nyuki umelahisisha kazi.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amesema kitaalamu Teknolojia hiyo ya kutumia drone ikisetiwa vizuri inauwezo wa kunyunyizia ekari moja kwa dakika sita na kuwataka wakulima kuitumia ili kuongeza idadi ya kilo wanazozalisha.
‘Tunataka uzalishaji wa zao la pamba kwa ekari moja ufikie kilo 1200 ili kuleta tija kwa mkulima,ambapo kwa sasa wakulima wengi wanapata kilo 250 hadi 300 tunataka tutoke huko na ndiyo maana serikali imekuja na teknolojia ya kisasa ya kutumia ndege nyuki”amesema Macha
Msimamizi wa zao la pamba kutoka Bodi ya pamba Wilayani Kishapu Thadeo Mihayo amesema kwa mkoa wa Shinyanga zipo drone saba lakini mipango iliyopo ni kuongeza zingine ili kufikia drone 14.
Mihayo amesema matarajio ya kulima zao la pamba kwa Wilaya ya Kishapu kwa msimu wa mwaka 2024/2025 ni ekari 220,000 na kwamba bodi ya pamba iko tayari na inaendelea kusimamia zao hilo kwa umakini.
Ofisa kilimo kupitia mradi wa jenga kesho iliyobora (BBT) Yombi Chedi amesema changamoto iliyokuwepo kwa wakulima wa kata ya Mwamalasa ni kukosa elimu ya kilimo bora kwani walio wengi walikuwa wakichanganya zao la pamba na mazao mengine.