SERIKALI YAENDELEZA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI

Serikali inaendelea na utekelezaji wa awamu ya Kwanza ya Mradi wa Maji Kaisho-Isingiro ambayo inahusisha ujenzi wa tanki lenye ujazo wa maji lita 225,000 pamoja na ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 17.

Ameyazungumza hayo Leo Aprili 29, 2025 Bungeni Jijini Dodoma Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Andrew Kundo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kerwa Innocent Bilakwate aliyeuliza Je, lini Awamu ya Pili ya Mradi wa Maji wa Rutunguru, Kaisho – Isingiro utaanza ili kuondoa adha wanayoipata Wananchi.

“Lengo la mradi huo ni kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi zaidi ya 37,500 waishio kwenye vijiji 11 vya Kaisho, Nyabishenge, Ibare, Ishaka, Karukwanzi A, Karukwanzi B, Kihanga, Kaitambuzi, Katera, Rutunguru na Nyakakoni.Utekelezaji wa awamu hiyo umefikia wastani wa asilimia 95 na unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2025,” amesema.

“Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kutatafuta fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi huo,” amesema Mhandisi Kundo.

Vilevile amesema chanzo cha uhakika cha fedha kwa Mfuko wa Taifa wa Maji kwa sasa ni tozo ya Shilingi 50 inayotokana na mauzo ya Mafuta ya dizeli na petroli.

“Aidha, pamoja na kuwepo kwa chanzo hicho, Serikali imeendelea kubuni vyanzo vingine vya kutunisha mfuko huo ikiwemo uwekezaji wa hati fungani na uandaaji wa maandiko ya miradi ili kupata fedha kutoka katika mifuko ya kimataifa ya kufadhili utekelezaji wa miradi ya maji ambapo kiasi cha Dola za Marekani Milioni 17.35 zimepatikana kupitia Dirisha la Mabadiliko ya Tabianchi la Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).”

“Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutafuta vyanzo vingi zaidi kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa fedha kwa Mfuko wa Taifa wa Maji ili uweze kutimiza majukumu yake ipasavyo,” amesema Mhandisi Kundo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *