Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, juhudi zinazofanywa na Wizara ya Nishati, Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) zimepelekea gharama za uletaji wa mafuta nchini (premium) kuendelea kushuka na hivyo kuchangia katika unafuu wa gharama za mafuta ikiwemo ya dizeli na petroli.
Amesema hayo tarehe 19 Januari 2024 jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ilipowasilisha taarifa kuhusu mwenendo wa biashara ya mafuta nchini kwa kipindi cha mwezi Septemba hadi Disemba 2023, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Kikao ambacho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Katibu Mkuu, Mhandisi, Felchesmi Mramba, baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na Watendaji wa Wizara ya Nishati.