Katika kuimarisha uchumi wa taifa kupitia ushirikiano imara kati ya sekta za umma na binafsi, Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi ili kuwezesha kukua kwa shughuli za kimaendeleo nchini na kuinua uchumi wa Taifa na mtanzania mmoja mmoja.
Akizungumza kwenye Mdahalo wa Kitaifa wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), uliofanyika jijini Mwanza, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, amesema kuwa serikali itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa sekta binafsi katika safari ya maendeleo ya taifa, hususan kuelekea dira ya Taifa ya mwaka 2050.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kua mshiriki wa karibu wa kuweka mazingira bora, wezeshi na shindani kwa sekta binafsi kufanya kazi kwa ufanisi,” alisema Nyongo mbele ya wadau mbalimbali wa maendeleo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha PPP, David Kafulila, amesema kuwa ni wakati muafaka kwa taifa kuwekeza kwenye uelewa mpana wa ubia kati ya sekta binafsi na serikali, ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati unakuwa wa ufanisi na wenye tija kwa wananchi.

“Kuna umuhimu wa kutekeleza miradi ya umma kwa utaratibu wa ubia, maswala ya ubia yamekua miongoni mwa ajenda kubwa kwenye mijadala ya uchumi duniani”
Akizungumza katika mdahalo huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala msaidizi sehemu ya Miundombinu Mhandisi, Chagu Ng’h’oma, amesema Mkoa wa Mwanza ni kitovu muhimu cha uchumi wa Kanda ya Ziwa kutokana na nafasi yake ya kipekee kijiografia na uwepo wa Rasilimali hiyo.

“Mwanza ni lango kuu la biashara ndani na nje ya nchi kupitia Ziwa Victoria. tunawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika uchumi wa bluu hasa uvuvi, usafirishaji majini, na utalii wa ziwani pamoja na sekta ya ufugaji wa kisasa wa samaki kwa njia ya vizimba,”
Katika hatua nyingine Chagu ameongeza kuwa Serikali ya Mkoa wa Mwanza imeweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, bandari, na maeneo ya viwanda, ili kuhakikisha miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi inatekelezwa kwa ufanisi.

Mdahalo huo umeandaliwa na Kituo cha Ubia (PPP Center) na kuwakutanisha wadau kutoka serikalini, sekta binafsi, taasisi za kifedha, mashirika ya kimataifa pamoja na wawekezaji binafsi kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu nafasi ya ubia katika kuleta maendeleo endelevu, huku pia ukilenga kutoa majibu ya pamoja kuhusu mwelekeo wa Dira ya Taifa 2050.
