SERIKALI YAAHIDI KUENDELEZA UBORESHAJI MIUNDOMBINU, HUDUMA ZA AFYA KWA WAZEE WASIOJIWEZA

Na Faustine Kasala – Kigoma.

Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya maisha ya wazee wasiojiweza nchini kupitia utoaji wa Bima ya afya na uboreshaji wa miundombinu ya makazi yao ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wa wazee kwenye jamii.

Akizungumza baada ya kutembelea Kituo cha Makazi ya Wazee Wasiojiweza cha Silabu kilichopo Kata ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema wazee wanapaswa kuthaminiwa na kuheshimiwa kwa kuwa wameendelea kuwa nguzo muhimu katika jamii.

“Nitumie nafasi hii ya uwepo wangu leo hapa katika makazi ya wazee hawa wasiojiweza kuwaambia kuwa Serikali ipo pamoja nanyi, tunatambua mchango wenu katika Taifa na jamii kwa ujumla hivyo tutaendelea kuboresha mazingira, Miundombinu ya makazi yenu, zaidi ni utowaji wa huduma za afya kwenu kwa njia ya Bima,” alisema Mahundi.

Awali, Afisa Ustawi wa Jamii na Msimamizi wa Makazi ya Wazee wasiojiweza Silabu, Binura Abbas Joshua, amesema kituo hicho kinaendelea kuwahudumia wazee kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, wakiwemo shirika la Joy in The Harvest lililopo Mkoani Kigoma ambao wamekuwa wakichangia huduma mbalimbali kwa ustawi wa wazee hao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Chuachua, ameipongeza Serikali kwa juhudi zinazoendelea kufanyika katika kuwahudumia wazee wasiojiweza, ikiwemo kuwawezesha kupata huduma za afya, chakula na mavazi.

Kituo cha kulea na kutunza wazee wasiojiweza cha SILABU Kilichopo Kata ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji, kina Jumla ya Wazee 22, Wanawake 10 na Wanaume 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *