SERIKALI YAAGIZA UTATUZI WA HARAKA MGOGORO ENEO LA MPAKA SINGIDA, MANYARA

Na Saulo Stephen – Singida.

Hatua za haraka zimetakiwa kuchukuliwa, ili kumaliza mgogoro wa mipaka unahusisha Mkoa wa Singida na Manyara katika eneo la mpaka wa mikoa hiyo miwili lililopakana na Hifadhi ya Msitu wa Mgori inayosimamiwa na Wakala wa Hifadhi za Misitu Tanzania (TFS).

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo amewataka wataalamu wa Ardhi kutoka Mkoa wa Singida kushirikiana na wenzao wa Mkoa wa Manyara kwenda uwandani kwa ajili ya kutafsiri ya alama za mipaka zinazotenganisha wilaya na mikoa hiyo na kutaka kazi hiyo kukamilika ifikapo Mei 30, 2026.

Ameeleza kuwa, baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, hatua inayofuata ni kuandaliwa kwa hati miliki za ardhi ili kuondoa kabisa migogoro ya mara kwa mara katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Kaspar Mmuya amemwagiza Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani, Bw. Hamdun Mansoor, kusimamia zoezi la kubaini na kutafsiri alama za mipaka pamoja na ramani za wilaya husika ili kuhakikisha kunakuwepo na uhalisia wa mipaka hiyo.

Mgogoro huo unahusisha Wilaya za Singida na Ikungi katika Mkoa wa Singida, Wilaya ya Hanang’ katika Mkoa wa Manyara, pamoja na Wilaya ya Chemba katika Mkoa wa Dodoma. Maeneo hayo yanazunguka Hifadhi ya Msitu wa Mgori yenye ukubwa wa hekta 39,931.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Hanang’, Mbunge wa jimbo hilo, Asia Halamga, amesema utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho utasaidia kupatikana kwa suluhisho la kudumu na kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji bila migogoro ya ardhi.

Vijiji vya Pohama na Nduamughanga katika Wilaya ya Singida, pamoja na vijiji vya Gorimba, Diloda na Murumba katika Wilaya ya Hanang’, vimekuwa na mvutano wa muda mrefu kuhusu mipaka hali ambayo imekuwa ikikwamisha shughuli mbalimbali za maendeleo kuendelea.

Hatua hizi zinatarajiwa kuimarisha usimamizi wa ardhi, kulinda Hifadhi ya Msitu wa Mgori na kuweka mazingira bora ya maendeleo kwa wananchi wa maeneo husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *