Na Saulo Stephen – Singida.
Serikali Mkoani Singida, imesema itaendelea kushirikiana na vyama vya ushirika, ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga wakati akiongea kwenye mkutano wa jukwaa la tatu la maendeleo ya vyama vya ushirika mkoa wa Singida.

Amesema, katika kuendeleza ushirikiano huo mkoa wa Singida ataendelea kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima na wanaushirikia mkoani humo ili kuendeleza shughuli zao za kilimo kwani sekta hiyo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa huo kupitia mazao kama, Alizeti, Vitunguu na Dengu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe akizungumza katika jukwaa hilo amesema wilaya ya singida ipo tayari kuunga mkopo jitihada za Serikali kwa kuhakikisha inawapa ushirikiano wa hali na Mali wanachama wa vyama hivyo kutoka wilaya ya Singida.

Nao baadhi ya washiriki kutoka vyama mbalimbali vya ushirika Mkoani Singida wamesema wamepokea kwa furaha ahadi hiyo ya ushirikiano kutoka kwa Serikali ya mkoa wakiamini kuwa hali hiyo itasaidia kuleta maendeleo zaidi kwa vyama hivyo mkoani humo.
