Serikali Mguu Sawa Uwezeshaji Sekta Ya Uvuvi

Na Costantine James,Geita

Serikali imesema imejipanga kikamilifu kuhakikisha wafanyabiashara wa samaki pamoja na wavuvi nchini wananufaika vyema na kazi wanayoifanya kwa kuwajengea mazingira rafiki ya kazi ikiwemo kuwatengenezea masoko ya uhakika ya uuzaji wa samaki kwa bei stahiki hatua itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi hali ambayo itaongeza mwamko wa wananchi kujikita zaidi katika sekta ya uvuvi.

Hayo yamebainishwa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wananchi wilayani Chato katika viwanja vya stendi ya zamani wilayani humo mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa soko la samaki la kisasa la “Chato Beach” uliogharimu zaidi ya Bilioni 1.7 ambapo amesema soko hilo litawasaidia wavuvi pamoja wafanyabishara hasa wa samaki kuwa na eneo la uhakika la kuuzia samaki wao.

Akitoa taarifa za Ujenzi wa Mradi huo, Meneja wa Mradi Mhandisi George Paul amesema Mradi umefikia hatua ya umaliziaji na unatarajiwa kukamilika rasmi Agosti 2,2024 ukitarajiwa kuwanufaisha zaidi wavuvi pamoja na wafanyabiashara ya samaki,kuzalisha ajira zaidi ya 1800 na kutengeneza soko la uhakika la samaki pamoja na kupunguza upotevu wa mazao ya samaki.

Nae Mbunge wa Jimbo la Chato Dkt. Medard Kalemani ametumia nafasi hiyo kuishukuru serikali kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo ambao ameeleza kuwa unakwenda kuwa lulu kwa wakazi wa wilaya ya Chato wanaojihusisha na shughuli za uvuvi kwa kuwangizia kipato.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *