SERIKALI KUTUMIA ZAIDI YA BILIONI 26 UJENZI WA SOKO LA KISASA BARIADI

Na Saada Almasi, Bariadi – Simiyu.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 26 kwa ajili ya kujenga soko kuu na la kisasa wWilayani Bariadi mkoani Simiyu ikiwa ni muendelezo wa kuboresha masoko ya miji nchi nzima.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Bunamhala na Isanga zilizoko mjini Bariadi Mbunge wa jimbo la Bariadi mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Andrea Kundo Mathew amesema kuwa matarajio ya kila mwananchi ni kuona maendeleo na katika vitu ambavyo havikuwa na sura nzuri ya mji ni pamoja na miundombinu ya soko kuu ambalo linategemewa na wananchi na ndiyo maana serikali imeamua kusikia kilio cha wananchi hao.

“natumia nafasi hii kumshukuru Rais wa nchi kwani Bariadi ya miaka mitano iliyopita haikuwa hii mnayoiona kuna mapinduzi makubwa ambayo hayakuwepo awali na kama mnakumbuka kipindi nimekuja kumuombea kura hayati Magufuli mlinishika mkono na kuniambia kuwa mnahitaji soko la kisasa na kwa kuwa tuna serikali sikivu leo hii tumepewa Bilioni 26 za ujenzi wa soko hili”amesema Mhandisi Kundo.

Akizungumzia baadhi ya miradi ya kimaendeleo iliyotekelezwa katika uongozi wake mhandisi Kundo amesema kuwa hadi sasa zaidi ya Bilioni 93  zimetotewa kutekeleza mradi wa maji,afya ,barabara na elimu akisema kuwa hizo zote ni juhudi za kimapinduzi za serikali kwa wananchi ili kuwafuta machozi ya kilio cha maendeleo katika maeneo yao.

“tumewaletea huduma muhimu za kijamii kama ule mradi wa maji wa shilingi BilIioni 5.01,mradi wa afya wa shilingi milioni 724, elimu msingi  572 ambapo shule zimejengwa na zinatoa elimu pamoja na ule wa ujenzi wa shule za sekondari wa Bilioni 6 na milioni 412,hayo ni mapinduzi makubwa na bado kuna maeneo ambayo bado umeme haujafika niwahakikishie kwamba tunakwenda kumaliza changamoto hizo ili kilio kisiendelee kwa wakazi wa maeneo hayo”ameongeza mhandisi Kundo.

Jambo FM imezungumza na baadhi ya wakazi wa Isanga Suzan Masanja na Daudi Bezekegwa ambao wameishukuru serikali kwa maendeleo hayo kwani hapo nyuma walipata  adha kubwa zilizochukua muda wao.

“sisi wanawake tunashukuru sana mradi huu wa maji umekuwa msaada mkubwa kwani tuna uhitaji mkubwa wa maji katika kunyweshea mifugo na matumizi ya nyumbani kipindi zcha nyuma ilikuwa hadi ukatafute maji ya visima lakini sasa maendeleo tunayaona,” amesema Suzan.

Kwa upande wake Daudi amesema kuwa baada ya kuisikia kauli ya Rais wan chi juu ya maboresho ya umeme amefarijika kwani tatizo la kukatika katika kwa umeme limekuwa likitatiza shughuli zao za kiuchumi na kuwarudisha nyuma kimaendeleo.

Hii ni ziara ya kawaida ya Naibu waziri wa maji na mbunge wa jimbo la Bariadi Mjini ya kueleza utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi hasa katika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

One response to “SERIKALI KUTUMIA ZAIDI YA BILIONI 26 UJENZI WA SOKO LA KISASA BARIADI”

  1. Haya ndiyo maendeleo,ki msingi ndani ya miaka 5 hii Bariadi imebadilika Kwa haraka sana yote haya ni kutokana na Mbunge aliyepo Mhandisi Kundo maana hata hapo awali Mbunge alikuwepo ambaye si Eng.Kundo ila hakukuwa na Kasi kama hii ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *