Serikali inatarajia kutoa waraka utakao waelekeza wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutekeleza miongozo inayowahusu watumishi wa Umma wenye ulemavu ili wapate mazingira rafiki na wezeshi wanapotekeleza majukumu yao.
Kauli hiyo, imetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba alipomwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa katika ufunguzi wa kikao cha wajumbe wa baraza la Taifa wa Chama cha Walimu Tanzania ambao ni wawakilishi wa walimu wenye Ulemavu.

Amesema, “Serikali itatoa waraka kuwakumbusha wakurugenzi wote nchini kutekeleza miongozoinayowahusu watumishi wa umma wenye ulemavu na niziombe taasisi na mashirika ya kitaifa na kimataifa kuendelea kufanikisha upatikanaji wa vifaa visaidizi kwa watumishi wa umma na wanafunzi wenye ulemavu.”
Katimba pia amewakumbusha viongozi wa vyama vya siasa kutoa nafasi kwa watu wenye Ulemavu wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili waingie kwenye vyombo vya maamuzi kwa ustawi na maendeleo ya watu wenye ulemavu na taifa kwa ujumla.