Na Gideon Gregory – Dodoma.
Serikali imesema itatenga maeneo Maalumu ya uwekezaji kwa ajili ya Vijana kupitia program ya Youth Industrial Special Economic Zones ambayo itawawezesha vijana kupata ardhi kwa ajili ya kujenga viwanda (Industrial shades).
Hayo yameelezwa leo Aprili 16,2026 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2026/27 na kubainisha maeneo hayo yatatengwa katika maeneo Maalum ya Uwekezaji.
“Maeneo hayo yako katika mikoa ya Dodoma (Nala, Ekari 100), Singida (MusisiriIramba, Ekari 100), Pwani (Kwala, Ekari 20), Mara (Bunda, Ekari .

100), Ruvuma (Songea, Ekari 100) na Bagamoyo (Pwani, Ekari 20),”amesema.
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa vijana wataweza kuwekeza kama watu binafsi au kwa vikundi, na wataweza kushiriki katika sekta mbalimbali.
Katika hatua nyingine Prof. Mkumbo amebainisha kuwa Ofisi hiyo kwa kushirikiana na wadau itaandaa mkakati wa kuvutia uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya uunganishaji na utengenezaji wa magari.
“Hitaji hili limetokana na tathmini ya awali iliyofanywa na Ofisi kwa kushirikiana na Taasisi ya Africa Association Automotive Manufacturer .

(AAAM) ya Afrika ya Kusini ambayo ilionesha fursa kubwa ya kuvutia wawekezaji katika sekta hii,”amebainisha.
Amesema Mkakati huo utaainisha aina ya wawekezaji wanaolengwa, aina ya uzalishaji unaokusudiwa, pamoja na vivutio vitakavyowekwa ili kuhakikisha ushindani wa sekta hiyo katika ngazi ya bara la Afrika.
“Dhamira ni kuwa, ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe miongoni mwa vinara wa uzalishaji wa magari katika bara la Afrika,”amesema.


