SERIKALI KUTAFITI MAENEO YENYE VIASHIRIA VYA MADINI NCHINI

Na Adam Msafiri, Musoma – Mara.

Serikali nchini, inapanga kufanyia utafiti eneo lenye ukubwa wa zaidi ya asilimia 50 hadi ifikapo mwaka 2030, ili kubaini maeneo yote yenye viashiria vya uwepo wa madinini na kuwarahisishia Wananchi waliojiajiri kwenye sekta ya madini hususan wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa ufanisi na uhakika.

Hayo yamesemwa Juni 6, 2025 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati akihitimisha kongamano la maonesho ya sekta ya madini mkoani Mara,lililoandaliwa na serikali ya mkoa huo kwa kushirikiana na wadau wa madini lililokuwa na lengo la kuonesha fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta hiyo.

Aidha Waziri huyo wa madini amesema, Mpaka hivi sasa nchi yetu imefanyiwa utafiti wa kina wa kubaini viashiria vya madini kwa asilimia 16 tu,Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuja na mpango kwamba ifikapo mwaka 2030 tuwe tumefanya utafiti wa kina wa eneo la nchi lenye ukubwa wa zaidi ya asilimia 50 ili Watanzania waweze kuongozwa vizuri.

Mavunde ameongeza kuwa, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anataka kuwatoa wachimbaji wadogo kwenye kuamini kwamba ukichinja kondoo,damu ya kondoo ukainyunyizia kwenye eneo unalochimba itaaidia kupatikana dhahabu kwa haraka tunataka kuwatoa wachimbaji wadogo kwenye kupiga ramli,tunataka kuwaongoza wachimbaji wadogo vizuri,” amesema Mavunde.

Katika hatua nyingine amesema tayari serikali ipo katika mpango wa ununuzi wa ndege maalumu itakayotumika katika shughuli za utafiti wa kubaini viashiria vya madini,kwa kupiga picha zaidi ya kilomita moja kwenda ardhini ili kuvumbua miamba yenye madini,hali itakayoongeza tija katika uchimbaji na kuwa na uchimbaji madini wenye uhakika.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema mkoa huo kwa sasa unatambulishwa zaidi na sekta ya madini na kwamba sekta hiyo kwa mwaka inachangia zaidi ya asilimia 18 kwenye pato la mkoa huku lengo likiwa ni kuifanya angalau ichangie asilimia 40 kwa mwaka.

Mara kwa sasa tunasomeka kuwa ni mkoa wa pili kwa uzalishaji wa madini lakini nikuhakikishie mheshimiwa Waziri,siku si nyingi wale ndugu zetu wa Geita tutawapiku na wao watatufuatia sisi katika eneo hilo la uzalishaji wa madini,” amesema Mtambi.

Nao wachimbaji wadogo walioshiriki kongamano hilo,wamedai kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya madini,ambapo wamesema kwa sasa serikali imetengeneza mazingira mazuri ya wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa uhuru na amani pamoja na kusaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa migogoro katika maeneo ya migodi.

Naye Mwenyekiti Taifa wa Chama cha wachimbaji wadogo John Bina amesema, zamani ilikua maeneo yote ya uchimbaji yanamikiliwa na wageni kutoka nje,lakini tangu Waziri Mavunde uingie Ofisini cha kwanza ulitenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo,pia zamani tulituhumiwa kuwa tunatorosha madini lakini sasa serikali ya awamu ya sita imejenga masoko kila kona”.

Kongamano la maonesho ya sekta ya madini mkoani Mara,limekwenda sambamba na matembezi makubwa yaliyoongozwa na Waziri Anthony Mavunde pamoja na Mkuu wa mkoa huo Kanali Evans Mtambi,ikiwa ni sehemu ya kutuma ujumbe wa kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassa kwa kazi nzuri anayofanya hususan katika kuihudumia na kuijali sekta ya madini nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *