Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amesema serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 9.167 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa eneo la Mindu, Manispaa ya Morogoro, waliopisha ujenzi wa Bwawa la Mindu.
Akijibu swali la Mbunge wa Morogoro Mjini bungeni, Naibu Waziri amesema wananchi waliopaswa kulipwa fidia wamegawanywa katika makundi mawili, ambapo kundi la kwanza linahusisha wananchi wasiopungua 500 waliokwisha kufanyiwa tathmini ya mali zao.

Mhandisi Kundo ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi la uthamini, jumla ya shilingi bilioni 4.8 zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi waliopo katika kundi la kwanza, na malipo hayo yanatarajiwa kuanza kutolewa mara taratibu za kifedha zitakapokamilika.

Aidha, Mhandisi Kundo amebainisha kuwa kuna hatua nyingine za uendelezaji wa mradi huo ikiwemo upanuzi na uinuliwaji wa kingo za matuta ya bwawa, hatua ambayo itasababisha wananchi wengine zaidi kuathiriwa na hivyo kulazimu kulipwa fidia.
Amesisitiza kuwa serikali imepanga kuhakikisha wananchi wote wa Mindu wanaoathiriwa na mradi wa ujenzi na upanuzi wa Bwawa la Mindu wanalipwa fidia zao zote kwa mujibu wa sheria, ili kuondoa malalamiko na kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa amani na manufaa kwa jamii.


