Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Ashatu Kijaji amesema changamoto ya kuchanja mifugo kidogo kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa, mashamba makubwa na hata kwa mfugaji mmoja imekua ndiyo chanzo cha kushindwa kuleta tija ya kutokomeza magonjwa yanayosumbua Mifugo kwa Taifa.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo leo Desemba 18,2024 Jijini Dodoma wakati akizindua Kampeni ya Chanjo za Mifugo Kitaifa itakayo tekelezwa kwa miaka mitano 2024-2029 ambapo Shilingi Bilioni 28.1 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mpango huo unaolenga kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya mifugo nchini.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhia kugharamia mpango wa chanjo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2024 hadi 2029 wenye thamani ya Shilingi Bilioni 216 kwa ajili ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo kote nchini na mpango huu tutaanza Januari 2025 ambapo katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 Serikali imetenga Shilingi Bilioni 28.1 kuchanja mifugo dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya ng’ombe, Ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Ugonjwa wa Mdondo wa Kuku ili kuwasaidia wafugaji wetu kote Nchini” alisema Dkt. Kijaji.
Aidha ameongeza kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuwasaidia wafugaji kufuga kwa tija ikiwemo utolewaji wa chanjo huku akiongeza kuwa endapo wakifanikiwa katika mpango huo taifa litaweza kupanua wigo wa kuuza mifugo na nyama nje ya nchi pamoja na maisha ya wafugaji kuboreka.
Dkt. Kijaji amesema awamu ya kwanza ya mpango huo wa chanjo Serikali kupitia wataalamu wa Sekta ya Mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa itachanja ng’ombe 19,097,223 dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya ngo’mbe (CBPP), Mbuzi na Kondoo 20,900,000 dhidi ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (PPR) na Kuku wa asili 40,000,000 dhidi ya Ugonjwa wa mdondo wa kuku (ND) ambapo lengo la serikali ni kutoa chanjo kwa mifugo angalau asilimia 70 ya idadi ya mifugo husika kwa miaka mitano mfululizo.
“Lengo la serikali ni kuchanja mifugo kufikia angalau asilimia 70 ya mifugo husika ambapo kwa sasa hali ya uchanjaji kwa ng’ombe, Mbuzi na Kondoo ni asilimia 21, Kuku wa Kienyeji asilimia 40 na kuku wa kisasa ni asilimia 100, hivyo kampeni hii itasaidia kutokomeza magonjwa ya mifugo, kutoa ajira za muda mfupi kwa vijana na wanawake 3540 na kuongeza usafirishaji wa nyama nje ya nchi Kutoka asilimia 14 ya sasa na kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2029” alisema Dkt.Kijaji.
Amesema katika kufanikisha zoezi hilo la chanjo serikali itachangia nusu bei ya gharama za chanjo ili kuwarahisishia wafugaji kuchanja mifugo yao.
“Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa Serikali itachangia nusu ya bei kwa ajili ya chanjo kwa mifugo ambapo kwa upande wa Ng’ombe itachangia Shilingi 500, kwa upande wa mbuzi na kondoo itachangia Shilingi 300 na upande wa kuku itakchangia Shilingi 100 itakuwa sawa na bure” aliongeza Dkt. Kijaji.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema Zoezi hilo la chanjo litahusisha wataalam na wafugaji ambapo katika kufanikisha zoezi hilo amewaomba wataalam na wafugaji kutoa ushirikiano.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Taifa CCWT Mrida Mshota amesema zoezi la chanjo linalokuja kwa awamu hii litawasaidia mafugaji hasa kukabiliana na magonjwa yanayoikabili mifugo na kuiomba Wizara kuupa kipaumbele pia ugonjwa wa Miguu na midomo (FMD).
“Naomba kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania kuipa uzito na kipaumbele Sekta ya Mifugo kwani imeonesha nia ya kutaka kutusaidia sisi wafugaji,”amesema.