SERIKALI KUENDELEZA UTENGEZAJI MAZINGIRA WEZESHI KWA NGO’s SHINYANGA

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Serikali MkoaniShinyanga, imesema itaendelea kutengeneza mazingira wezeshi kwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO’s), ili yaweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na mipango ya serikali pamoja na kuhakikisha miradi inayotekelezwa na mashirika hayo inaendana na mahitaji halisi ya wananchi na vipaumbele vya serikali.

Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi wakati akifungua kongamano  la jukwaa la mwaka  la mashirika yasiyo ya kiserikali, lililofanyika hii leo Septemba 3, 2026 mjini Shinyanga, likikutanisha NGO’s zilizosajiliwa katika mkoani humo.

Amesema, NGO’s  zinapaswa kuweka fikra mpya  na ubunifu, ili kujenga ubia na kutumia fursa mbalimbali zilizopo Shinyanga, kwani mashirika hayo ni sehemu ya wadau wa maendeleo  kwa kushirikiana na serikali katika kutekeleza miradi ikiwemo ya afya elimu, mazingira, uwezeshaji wa wanawake na vijana na ustawi wa jamii ikiwa ni pamoja na kupunguza umasikini na kufungua fursa za kiuchumi.

Aidha, amesema mashirika yasiyo kwa kiserikali ndani ya mkoa wa Shinyanga   yana wajibu mkubwa katika kutekeleza dira ya taifa ya 2050 ambayo imewapa wadau wa maendeleo nafasi kubwa katika kutimiza utekelezai wake  na kwamba mashirika hayo hayana budi kushirikiana na idara pamoja na vitengo vilivyopo ndani ya mkoa wa Shinyanga na halimashauri zote sita kuyafikia malengo ya dira hiyo ambayo utekelezaji wake umeanza Julai 2026.

Akitoa mada katika kongamano hilo, Msajili Msaidizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Shinyanga, Rehema Edson ameyataka mashirika hayo yasiyokuwa ya kiserikali  kufata maadili na  sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kuwa na uwazi katika suala zima la Mapato yanayotokana na wafadhili  na kuanisha aina ya wafadhili wanaowawezesha na kuweka wazi   mahali walipo ili kuondoa sintofahamu inayokuwepo juu ya uendeshaji wa mashirika hayo.

Rehema pia ameyataka mashirika hayo kulipa ada za usajili kwa wakati pasipo kusumbuana na serikali,pamoja  na kutekeleza miradi endelevu kwa wananchi,hata pale shirika  husika  lisilo la kiserikali linapomaliza muda wa utekelezaji wa mradi , uweze kuendelea kuwanufaisha wananchi.

Kwa upande wake mwakilishi baraza la taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali  Bakari Kibile amesema mashirika hayo katika siku za nyuma  yamekuwa yakikumbwa na changamoto ya kukosa uwakilishi katika vikao vya kimaamuzi  vya serikali, lakini kwasasa hali imebadilika kumekuwa na uwakilishi  wa wajumbe kutoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali kuanzia ngazi ya halimashauri mpaka mkoa.

Amesema, mashirika hayo yasiyo ya kiserikali yataendelea kushirikiana na serikali katika kuhudumia wananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kufata sheria kanuni na miongozo ya serikali katika utekelezaji wa majukumu ili malengo yaliyoainishwa katika DIRA ya maendeleo ya 2050 kupitia wadau wa maendeleo yaweze kufikiwa na jamii iweze kunufaika.

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) ni taasisi zinazoundwa na watu au makundi ya watu kwa lengo la kushughulikia changamoto mbalimbali za kijamii, kiuchumi, kiafya na kimazingira bila kuwa sehemu ya serikali. Mashirika haya hufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi, serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Katika jamii, NGOs zina mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya, elimu, uwezeshaji wa vijana na wanawake, utunzaji wa mazingira, kupunguza umaskini na kulinda haki za binadamu. Pia hutoa elimu na uhamasishaji kuhusu masuala mbalimbali yanayoathiri maisha ya wananchi.

Hata hivyo, mashirika haya yanakabiliwa na changamoto ikiwemo uhaba wa fedha, utegemezi wa wafadhili, mazingira magumu ya utekelezaji wa miradi na wakati mwingine ukosefu wa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa jamii.

Kwa ujumla, NGOs ni wadau muhimu katika maendeleo ya jamii, ambapo  Ushirikiano mzuri kati ya mashirika hayo, serikali na wananchi unaweza kusaidia kuongeza ufanisi wa miradi na kuleta maendeleo yenye manufaa kwa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *