SERIKALI KUENDELEZA MAZINGIRA WEZESHI VIKUNDI NUFAIKA MIKOPO YA HALMASHAURI

Na Tryphon Odace – Kigoma.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, ambaye pia ni Mbunge viti maalumu Mkoa wa Kigoma, Zainabu Katimba amesema, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vinavyonufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri, ili kuendelea kuwainua kiuchumi.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea vikundi vinavyonufaika na mikopo katika Manisppaa ya Kigoma Ujiji, Katimba amesema mikopo inayotolewa kupitia Halmashauri ni sehemu ya jitihada za Serikali kuwawezesha wananchi, hususan vijana, wanawake na makundi mengine, kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi.

“Serikali itaendelea kutoa mikopo hiyo na kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya kutumia mitaji hiyo katika shughuli za uzalishaji” amesema Katimba.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambaye pia ni mwezeshaji wa wananchi kiuchumi, Jabiri Majira amesema wanaendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi, hasa vijana, kujiunga katika vikundi na kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri.

Amesema, pamoja na kutoa hamasa wanaendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia masharti ya mikopo, matumizi sahihi ya fedha pamoja na urejeshaji kwa wakati ili fursa hiyo iwe endelevu na kwa watu wengine.

Hata hivyo, baadhi ya wanavikundi walionufaika na mikopo hiyo wameeleza kuwa imekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha kuongeza mitaji na kupanua shughuli zao za kiuchumi.

Vikundi vilivyotembelewa na Katimba ni pamoja na cha Women Group kilichopo kata ya Mwanga kaskazini kinchojihusisha na ushonaji wa mashuka, Kikundi cha Lukundo kilichopo kata ya Buhanda, Kikundi cha ufangaji kuku na mnufaika wa mikopo hiyo ambaye ni mlemavu vyote vikiwa ndani ya manispaa ya Kigoma Ujiji.

Serikali, imekuwa ikitoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwa makundi mbalimbali, huku ikiweka msisitizo katika usimamizi na utoaji wa elimu kwa wanufaika ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *