
Na Saada Almasi -Simiyu
Katika kuendelea kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini serikali imeona kuna haja ya kubadili uelekeo wa mfumo wa elimu unaotolewa na kuhamia katika utoaji wa elimu ya Amali ili mwanafunzi anapotoka shuleni awe na ujuzi utakao mfanya aweze kujiajiri na kuajiriwa katika sekta binafsi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa shule ya sekondari ya Amali ya Mwamapala iliyoko wilayani Itilima mkoani Simiyu Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amesema kuwa hapo awali elimu iliyotolewa iliacha vijana watafute ajira na kukaa bila kazi lakini sasa mwanafunzi atatoka shuleni akiwa na ujuzi utakao muongoza.
“Elimu iliyotolea ilimuacha kijana akiwa hana ajira wala hawezi kujiajiri na kugeuka changamoto kwa serikali kwa kuongeza uhitaji wa ajira nchini lakini elimu hii itamuuza kwenye soko la ajira lakini yeye mweyewe ataweza kutumia ujuzi wake kujiajiri”amesema Rais Samia.

“Tunashukuru Mungu ametupa vijana wengi Tanzania lakini kama nchi haina uwezo wa kuwaajiri wote ndio maana tumeamua kuwapa ujuzi ili waweze kuwa mafundi wanaoweza kuajiriwa na kujiajiri katika sekta binafsi kwa kuwa sekta binafsi inakuwa kwa kasi hapa nchini”ameongeza Rais Samia
Aidha Rais Samia amewataka wananchi mkoani humo kuwapa nafasi Watoto wao ya kupata elimu kwani serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya elimu kwa kuongeza shule za msingi,sekondari,vyuo vya ufundi pamoja na kufungua matawi ya vyuo vikuu ili Watoto engi zaidi wapate haki ya elimu
“Serikali inatoa pesa nyingi katika kujenga shule za msingi ,sekondari za ufundi na sasa tumeanza kuleta matawi ya vyuo vikuu nia na madhumuni ni kumpa fursa kila mtoto ya kupata elimu sasa niwaombe wazazi waacheni Watoto wenu wapate elimu,na katika shule hii tunaweka mpango mzuri wa vifaa vya kufundishia ili hadi kufika mwezi Januari mwakani Watoto waanze kupata elimu”amesema Rais Samia
Naye waziri wa elimu Aldoph Mkenda amesema kuwa shule za amali zinatofautiana kulingana na mchepuo kwani zipo za kilimo,ufundi ,michezo na kwamba mageuzi ya elimu si kitu cha kuonekana kwa macho mara moja ni suala la muda kuonyesha matokeo ya uwekezaji
“hii ni shule ya amali tutakayotoa mafunzo ya ufundi stadi lakini zitakuwepo nyingi za masomo tofauti mfano michezo,kilimo, Sanaa ambazo zote zitamfanya mwanafunzi amalize akiwa na ujuzi japokuwa hii falsafa aliyokuja nayo Rais wetu ni mageuzi ya elimu si kitu cha kuonekana mara moja matokeo yake mtakuja kuyaona baadae”amesema Waziri Aldoph
Akimkaribisha Rais Dkt Samia katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo Waziri wa Nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mohammed Mchengerwa amesema kuwa ndoto ya kuanzishwa kwa shule za amali ilitoka kwa Rais Samian a yeye kama waziri akapokea maagizo ya kuanziasha shule hizo ili mwanafunzi atakaye hitimu aweze kujitegemea
“awali hili wazo alikuja nalo mheshimiwa Dkt Samia Suluhu na akalifikisha kwangu mara tu baada ya kuingia katika hii wizara nikiwa na waziri wa elimu na ulisema mhitimu anayehitimu elimu yake anatakiwa kuwa na uwezo wa kujitegemea,na ukatupatia zaidi ya shilingi bilioni 41.6 za ujenzi wa shule hizi nchi nzima”amesema Waziri Mchengerwa
Ujenzi wa shule ya Amali Mwamapalala imegharimu shilingi bilioni 1.6 ikiwa katika asilimia 90 ya utekelezaji na kutokana na kuridhishwa na hatua hiyo Rais Samia ametoa maagizo kwa makandarasi kukamilisha ujenzi kwa wakati ili Januari mwakani ianze kupokea wanafunzi