Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imekamilisha urekebu wa Sheria Kuu 446 za nchi na kuandaa Toleo la Sheria Zilizofanyiwa Urekebu la Mwaka 2023.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro ameyasema hayo jijiji Dodoma wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025 ambapo amesema toleo hili lilizinduliwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 23, 2025.
“Toleo hili litaanza kutumika tarehe 1 Julai, 2025, Hatua hii ni sehemu ya jitahada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria na kuimarisha misingi ya utoaji haki. Toleo hili ni la pili tangu Nchi yetu ilipopata uhuru, Toleo la Kwanza lilitolewa mwaka 2002 na liliandaliwa kwa ufadhili Benki ya Dunia,” amesema.

Hata hivyo, amesema toleo la Sheria Zilizofanyiwa Urekebu la Mwaka 2023 limeandaliwa kwa fedha za ndani na wataalaam wa ndani.
Vilevile amesema Katika kuimarisha uratibu wa huduma za msaada wa kisheria katika ngazi ya Halmashauri, Kata, Vijiji na Mitaa, Serikali imeanzisha Madawati ya Msaada wa Kisheria katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 184.
“Jumla ya watumishi 449 wameajiriwa ili kuwezesha Madawati hayo kutekeleza majukumu yake ipasavyo, Kupitia madawati haya, Wananchi wanawasilisha malalamiko na changamoto zao za kisheria na kupatiwa ufumbuzi”, amesema
“Tangu kuanzishwa kwa Madawati ya Msaada wa Kisheria, jumla ya wananchi 6,427,738 Wanaume 2,905,356 na Wanawake 3,522,382 wamepatiwa elimu juu ya masuala ya kisheria na haki za binadamu”. Amesema